Wabunge waliofukuzwa Chadema wapo kwenye mikono salama - Spika Ndugai

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai amesema hakuna mahali anapobanwa kwamba ni lini awafukuze wabunge 19 waliofukuzwa uanachama Chadema, katika bunge hilo.

Kauli ya Spika Ndugai imekuja wakati kukiwa na shinikizo kutoka kwa viongozi na makada wa Chadema wakimtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati kwa kuhakikisha wabunge hao wanaondolewa, kwani kuwepo kwao bungeni ni kinyume cha Katiba.

Wabunge hao wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema, Halima Mdee walifukuzwa uanachama wa Chadema Novemba 27, 2020 baada kwenda bungeni kuapishwa kuchukua nafasi za viti maalum bila idhini ya chama hicho.

Akizungumza leo Mei 3 bungeni jijini Dodoma baada ya kipindi cha maswali na majibu, Ndugai amewataka wabunge hao wachape Kazi kwa kuwa wako mikono salama, huku akionya vyama viache kuwanyanyasa wanawake.

Akizungumzia utaratibu wa vyama kumwandikia barua, Spika Ndugai amesema kuna taratibu za kufuatwa kabla ya kuwafukuza wabunge hao.

"Makatibu wajifunze kuandika barua nzuri kwangu, huwezi kuniandikia kikaratasi hivi halafu unataka niwafukuze wabunge 19, hiyo siyo kazi yangu hata kidogo, ninyi wabunge chapeni kazi kwani mko kwenye mikono salama,"amesema Ndugai.

Hata hivyo amesema wabunge hao bado hawajasikilizwa Baraza Kuu la chama hicho na hivyo hawezi kuwaondoa watu ambao hawajapata kujitetea.

 

Post a Comment

0 Comments