Kamati ya Bunge yaridhishwa na Serikali kutoa elimu ya uvuvi 2 Bwawa la Mtera

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeridhishwa na elimu iliyotolewa kuhusu uvuvi haramu kwa wavuvi wa bwawa la Mtera.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dkt. Christine Ishengoma ameyasema hayo leo (19.06.2021) baada ya kamati kumaliza ziara yake kwenye kijiji cha Misisiri wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma na kijiji cha Mnadani wilaya ya Iringa ambapo walizungumza na wavuvi na wananchi wa maeneo hayo.

Dkt. Ishengoma amesema katika vijiji vyote walivyopita wamekuta wavuvi na wananchi kwa ujumla wanayo elimu kuhusu uvuvi haramu na wanashiriki katika kudhibiti kwa kukamata nyavu haramu na kuziteketeza.

Wavuvi wametakiwa kuendelea kudhibiti uvuvi haramu katika bwawa hilo ambalo kwa sasa samaki wamepungua katika baadhi ya maeneo kutokana na Uvuvi haramu.

Dkt. Ishengoma amewaahidi wananchi wa kijiji cha Mnadani kuwa atalifikisha tatizo la wingi wa viboko katika bwawa hilo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii ili aweze kulishighulikia.

Naye Katibu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa wizara imekuwa ikitoa elimu kuhusu uvuvi haramu na madhara yake kwa wavuvi na wananchi wanaolizunguka bwawa la Mtera ambapo kwa sasa wananchi hao wamekuwa wakishirikiana na serikali kudhibiti na kuteketeza nyavu zisizofaa zilizokamtwa.

Dkt. Tamatamah amewaahidi wavuvi wa kijiji cha Miseseri kuwaletea injini moja ya boti mwezi Julai, 2021 ambayo pamoja na shughuli za uvuvi itawasaidia katika kufanya doria za kudhibiti uvuvi haramu.

Pia amewaahidi wananchi hao kuwa atawatuma wataalam wa  utafiti kutoka TAFIRI kuja kuangalia kutafiti Kama upo uwezekano wa kuweka mbegu ya samaki ili kusaidia kuongeza wingi wa samaki katika bwawa.

Dkt. Tamatamah amewasisitiza wavuvi kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili waweze kukopesheka na kuweza kupata zana sahihi za uvuvi ambazo mara nyingine hutolewa na wizara.

Mkazi wa kijiji cha Mnadani kata ya Izazi wilayani Iringa, Bw. Amiri ameieleza kamagi hiyo kuwa viboko katika bwawa hilo wameongezeka na wamekuwa wakijeruhi na hata kuwauwa wavuvi na hivyo kusababisha wavuvi kutokwenda kuvua. Tatizo hili limefanya samaki kuwa wachache katika masoko na kuwafanya wavuvi kutafuta shughuli nyingine za kuwaingizia kipato na hivyo ameiomba kamati kuwasaidia kulitatua tatizo hilo.

Wananchi katika vijiji vyote viwili wameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge na wizara kwa kuwatembele na kusikiliza matatizo waliyonayo na wanaomani kuwa matatizo yao yatatafutiwa ufumbuzi.

 

Post a Comment

0 Comments