Rais Joe Biden leo anakutana na rais wa Afghanistan Ashraf Ghani pamoja na mshirika wake wa zamani wa kisiasa Abdullah Abdullah, kujadili uungaji mkono wa Marekani kwa taifa hilo wakati kundi la mwisho la wanajeshi wa Kimarekani likifunga virago baada ya miaka 20 ya vita na mapambano dhidi ya kundi la Taliban.
Rais Ghani anajaribu kukabiliana na kundi la Taliban ambalo limeanza kupata nguvu tena. Masuala mengine yatakayojitokeza ni pamoja na ongezeko la maambukizi ya Covid-19, na vita ya kisiasa huko mjini Kabul.
Biden ameliomba bunge kuidhinisha kiasi cha dola bilioni 3.3 kama msaada wa kiusalama kwa Afghanistan mwaka ujao na anatarajiwa pia kuipatia dozi milioni 3 za chanjo ya Covid-19. Mkutano wa leo unafanyika wakati mchakato wa amani ukikwama na vurugu zikizidi kuongezeka.
