Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wamekataa shinikizo la Ujerumani na Ufaransa, la kuanza tena mazungumzo na rais wa Urusi Vladimir Putin. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema badala ya mkutano wa kilele na Rais Putin, viongozi hao wameafikiana kuendeleza ''muundo wa mjadala na Urusi''. ''
Leo haikuwezekana kukubaliana kukutana na Putin na kutafuta suluhisho kwa ngazi ya mkutano wa kilele, lakini kwangu ni muhumu kuwa muundo wa majadiliano utaendelezwa. Binafsi ningependelea hatua pana zaidi, lakini hata hivi ni sawa tu, tutaendelea kuifanyia kazi".
Rai ya Ujerumani na Ufaransa imekabiliana na upinzani mkali wa nchi za mashariki mwa Ulaya, ambazo zinasema uhusiano baina yao na Urusi umezorota vibaya, na hazioni haja ya kuipa zawadi ya mazungumzo kabla ya kubadilisha mienendo yake ya kibabe.
Ujerumani na Ufaransa zilitoa pendekezo hilo la mkutano na Putin kufuatia mazungumzo baina ya kiongozi huyo wa Urusi na rais wa Marekani Joe Biden wiki iliyopita mjini Geneva.
Mkutano wa mwisho baina ya Putin na viongozi wa Umoja wa Ulaya ulifanyika mwanzoni mwa mwaka 2014.
