Kuelekea mchezo wa kesho wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho(ASFC), Simba dhidi ya Azam, makocha wa timu zote kila mmoja ametamba kutinga fainali ya michuano hiyo.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa kesho kwenye Uwanja kwenye dimba la Majimaji, Songea kuanzia saa 9:30 Alasiri.
Akizungumzia mechi hiyo leo, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, amesema malengo yao tangu msimu unaanza ni kutetea mataji yao yote mawili, ikiwamo la Ligi Kuu.
“Tangu mwanzo wa msimu lengo letu lilikuwa ni kutetea taji hili na sasa tumefika hatua hii kwa hiyo tumejipanga kushinda na kuingia fainali.
Gomes amesema mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa kikosi cha Azam, lakini hakuna wa kuwazuia kuingia fainali.
“Azam ni timu nzuri na tunakumbuka mchezo wa mwisho tulipokutana tulifanikiwa kumiliki mchezo ila tulipoteza nafasi nyingi hasa kipindi cha kwanza lakini tumejitahidi kuondoa mapungufu ili kupata ushindi,” amesema Gomes.
Kwa upande wake Kocha Msaidizi wa Azam, Vivier Bahati, amesema wametengeneza mbinu nzuri ya kukabiliana na wapinzani wao kuhakikisha wanaibuka na ushindi.
"Kesho watu wote wako tayari kupambana, tunaingia uwanjani na mbinu nyingi za kupata ushindi, tutashambulia na kujilinda pia," amesema Bahati.
