Jinsi msongo wa mawazo unavyosababisha mvi


Kadri umri wa mwanadamu unavyosonga kuongezeka, ni kawaida kwa nywele kubadili rangi na kuwa za kijivu au nyeupe.

Watu wengi hugundua kwamba mvi huanza kuota mapema miongoni mwa watu wanaofanya kazi zilizo na shinikizo sana kama vile miongoni mwa marais, maafisa wakuu watendaji na hata maafisa wakuu wa fedha.

Mpaka sasa hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba msongo wa mawazo humfanya mtu kuota kwa mvi mapema.

Lakini wataalamu wanasema hali ya kuota mvi mapema kunaweza kudhibitiwa.

Kulingana na utafiti mpya wa Chuo Kikuu cha Columbia uliochapishwa katika jarida la eLife: wakati chanzo cha mafadhaiko kinapoondolewa, nywele zinaweza kurudi kwenye rangi yake ya kawaida.

Kwanini Ghana haina 'wanawake wazee'?

Kwa miongo kadhaa tumejaribu kuelewa husiano uliopo kati ya msongo wa mawazo na kuota kwa mvi, na huu ndio utafiti wa kwanza ambao unaonyesha uhusiano wazi kati ya mfadhaiko wa kisaikolojia na nywele nyeupe" anasema Martin Picard, mtaalamu wamasuala ya kisaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Vagellos na mtafiti mweza katika uchunguzi huo.

Kwa kawaida, watu wa asili ya kizungu huanza kuota mvi wakiwa katika awamu yao ya mwisho ya miaka ya thelathini.

Wale wenye asili ya kihindi huanza kushuhudia hali hii mwanzoni mwa umri wa miaka ya 40, huku Waafrika wakianza kuota mvi kati kati ya miaka ya 40.

Nini kinachozipa nywele zako rangi?

Vifuko vidogo vya vinyweleo vilivyo na seli maalum za rangi huzingira nywele. Seli hizi za rangi zinaitwa melanini. Melanini huipa ngozi na nywele zako rangi. Muda unavyozidi kusonga, vinyweleo hivi vya nywele hupoteza rangi na kusababisha mvi.

Nini kinachosababisha mvi kuota mapema?

Kwa baadhi ya watu suala la nywele kubadili rangi huwa la kiukoo. Ikiwa wazazi au babu zako walikumbwa na tatizo hili, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba wewe pia utashuhudia haya. Kwa bahati mbaya, hakuna jambo ambalo laweza kufanywa kuepuka.

Upungufu wa virutubisho vya vitamini

Ukosefu wa virutubisho vya kutosha vya vitamin B12 mwilini pia waweza sababisha ngozi na nywele kubadili rangi. Aidha, upungufu huu waweza kusababisha hali ya upungufu wa damu mwilini (ambapo seli za damu hazina himoglobini ya kutosha, kiungo muhimu kinachobeba oksijeni mwilini).

Masuala ya homoni

Iwapo tezi dundumio (thyroid gland) haifanyi kazi ipasavyo, huenda uwezo wa mwili wako kuzalisha melanini ukapungua, na hivyo kusababisha nywele zako kubadili rangi mapema. Tezi dundumio ni kikoromeo kidogo kinachopatikana katika sehemu ya mbele ya shingo lako.

Maradhi yanayotokana na mwitiko wa kinga usio wa kawaida

Katika hali hii, mfumo wa kinga mwilini hushambulia seli zake. Kuna aina mbili katika kitengo hiki; alopecia areata na vitiligo ambazo zaweza sababisha nywele kubadili rangi mapema.

Mhusika akiwa na vitiligo, mfumo wa kinga mwilini hushambulia seli zinazozalisha melanini mwilini. Hii husababisha kuchipuka kwa madoa meupe kwenye ngozi na kuota kwa mvi mapema.

Ikiwa unakabiliwa na ugonjwa wa alopecia areata, nywele hutoweka ghafla na kuota tena na ni hapa ndipo mhusika anagundua kwamba nywele nyeupe zimechipuka.

Uvutaji sigara

Uvutaji sigara una madhara mengi ikiwa ni pamoja na saratani, maradhi ya moyo na mapafu. Aidha, uvutaji sigara unaweza kuhusishwa na kuota kwa mvi.

Rangi za kemikali na bidhaa zingine za nywele

Bidhaa za nywele zilizoundwa kwa kemikali ya 'hydrogen peroxide' zimeonekana kuwa na madhara kwa nywele na zaweza kusababisha kuota kwa mvi.

Kuna utafiti unaohusisha tatizo la nywele kubadili rangi mapema na wembamba wa mifupa (osteopenia) na maradhi ya moyo, lakini upelelezi zaidi unahitajika hapa.

Je, uotaji mapema wa mvi waweza kuzuiwa?

Ikiwa hali hii inatokana na jeni, basi jibu ni la. Itakubidi kuzoea mabadiliko ya rangi ya nywele zako.

Ikiwa una mvi kisha upake rangi, itakubidi kurudia utaratibu huu zikiota tena.

Ikiwa hauna uhakika iwapo matatizo yako ya kiafya yanasababisha kuota mapema kwa mvi, basi enda ufanyiwe uchunguzi wa mwili wote. Ikiwa kuna hali yoyote ya kiafya inayosababisha tatizo hili, basi litahitajika kuangaziwa.

Dumisha lishe bora hasa chakula kilicho na viwango vingi vya Vitamin B12: Vyakula kama vile mboga za kijani na vyakula jamii ya kunde kama vile maharagwe vitakufaa. Ikiwa upungufu wa Vitamin B12 mwilini mwako umekithiri, utahitajika kumeza vijalizo.

Mbinu zingine ni pamoja na kuacha kuvuta sigara mara moja. Pia, utahitajika kuchagua bidhaa za nywele kwa busara huku ukiepukana na kemikali zinazoathiri ngozi ya kichwani. Lakini ikiwa tayari una mvi, ni vigumu kurejelea hali ya kawaida

Post a Comment

0 Comments