https://monetag.com/?ref_id=TTIb Njia ya rahisi ya kujitibu mafua | Muungwana BLOG

Njia ya rahisi ya kujitibu mafua


Mafua ni ugonjwa unaosumbua watu wengi kila mwaka, hasa yanapoanza kutokea mabadiliko ya hali ya hewa, kutoka msimu wa joto kuingia baridi au kutoka msimu wa kiangazi kuingiza masika. Ili kujikinga na ugonjwa wa mafua, ni lazima mwili uwe na kinga ya kutosha.

Orodha ya vyakula vifuatavyo vimeelezwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuimarisha kinga ya mwili na kupambana na maambukizi mengine kwa kuwa na kiasi kikubwa cha protini na virutubisho vingine.

Supu ya kuku.

Supu ya kuku wa kienyeji inaelezwa kuwa na virutubisho vinavyosaidia kupunguza utokaji wa makamasi. Utapata virutubisho vingi zaidi ukitengeneza supu ya kuku kwa kuchanganya na mboga za majani. Weka chumvi kiasi kidogo katika supu hiyo.

Vitunguu saumu.

Vitunguu saumu vina kirutubisho aina ya ‘allicin’ ambacho kina uwezo wa kutoa kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ya kuambukiza. Kitunguu saumu kinatoa kinga halikadhalika kinapunguza muda wa mtu kuumwa na mafua. Tumia kitunguu hicho kwa kupika kwenye chakula au kwa kutafuna punje zake.

Chai.

Chai, hasa ya kijani, (green tea) ina virutubisho vya kuimarisha kinga ya mwili. Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na jarida moja la masuala ya virutubisho nchini Marekani (Journal of the American College of Nutrition) umeonesha kuwa watu wanaotumia chai kwa mpangilio maalum hawasumbuliwi mara kwa mara na mafua pamoja na magonjwa mengine ya kuambukiza, huwa salama na mafua au siku za kuumwa mafua hupungua kwa asilimia 36 ukilinganisha na wale wasiokuwa na kinga imara.

Hata hivyo, tahadhari inatolewa kwa watoto wa shule kutokupewa kiasi kingi cha chai kwa siku. Unywaji wa kikombe kimoja kwa siku kwa mtoto wa shule siyo mbaya. Kwa mtu mzima, asizidishe vikombe vitatu kwa siku. Ikumbukwe kuwa chai inapotumika kwa wingi kupita kiasi, huweza kusababisha pia tatizo la kukosa choo kwa muda mrefu.

Kunywa kiasi kwa afya yako.

Machungwa.

Utafiti unaonesha kwamba ulaji wa vyakula vyenye Vitamin C kwa wingi kila siku husaidia kuondoa au kuzuia ugonjwa wa mafua. Miongoni mwa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha Vitamin C ni pamoja na machungwa, mboga za majani aina ya Brokoli na pilipili kali.

Ili kupata kiasi kingi cha Vitamin C, inashauriwa machungwa yaliwe pamoja na nyama zake za ndani au kunywa juisi yake.

Asali

Kama inavyojulikana, asali ni tiba ya matatizo mengi ya kiafya, miongoni mwa hayo ni pamoja na mafua. Asali inasaida kuondoa kikohozi na muwasho kwenye koo.

Halikadhalika, asali inaweza kutumiwa na watoto wadogo kama dawa. Watoto wanaoruhusiwa kutumia asali kama tiba ni wa umri kati ya miaka 2 hadi 5.

Hawa dozi yao ni nusu kijiko kidogo cha asali, wenye umri wa miaka 6-11 wapewe kijiko kimoja kidogo na wenye umri kuanzia miaka 12 hadi 18, wapewe vijiko vidogo viwili vya asali wakati wa kulala.

Mtindi.

Kutokana na kiwango kikubwa cha protini ilichonacho, Mtindi ni chakula kingine kinachofaa kuliwa na mtu mwenye mafua ili kupunduza siku za kusumbuliwa na ugonjwa kukohoa.

Pweza.

Samaki aina ya pweza wana virutubisho vingi vya kuongeza kinga ya mwili yenye uwezo wa kupambana na bakteria pamoja na virusi vya mafua. Kiasi kidogo cha pweza, awe wa kukaangwa au kuchemshwa kama supu, anafaa kuliwa mara kwa mara kuimarisha kinga ya mwili.

Post a Comment

0 Comments