F Mkakati Kulinda Wananchi Na Madhara Ya Tumbaku | Muungwana BLOG

Mkakati Kulinda Wananchi Na Madhara Ya Tumbaku


MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Adam Fimbo anasema Serikali kupitia  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,  Jinsi, Wazee na Watoto, katika siku 100 za Rais Samia imeidhinisha TMDA kufanya udhibiti wa bidhaa za tumbaku 


Anasema jukumu hilo hawakuwa nalo na kwamba bidhaa hizo zilikuwa zinasimamiwa chini ya sheria ya kudhibiti bidhaa za tumbaku ya mwaka 2013 pamoja na kanunui zake za mwaka 2011.


“Maana yake ni kwamba sasa bidhaa hizo kama sigara na ugoro tumeanza kuwekea utaratibu wa kudhibiti ili kuokoa afya ya jamii kwa sababu tumbaku inahusishwa na magonjwa yasiyoambukiza na watu wengi wamekuwa wakiathirika.


“Kazi hiyo sasa tumeanza kufanya na lengo ni kulinda afya ya jamii… Kwenye dira yetu imebaki hivyo, kuwalinda watumiaji,” anaeleza.


Anasema bidhaa za tumbaku zinasababisha magonjwa kadhaa ikiwa ni pamoja na moyo, saratani, tatizo la mapafu na ugonjwa wa kisukari.


“Kazi yetu ni kuangali namna ambayo tutapunguza idadi ya watu wanaotumia tumbaku na vile vile kazi yetu ni kuhakikisha watu wapya ambao hawajawahi kuvuta sigara wasianze,” anasema.


Anasema katika muktadha huo watoto wenye umri chini ya miaka 18 ambao sheria inakataza wasuvute sigara TMDA inaweka mazingira ya kuhaikisha kwamba hawatumbukii kwenye uvatji wa sigara au kula ugoro.


“Tumeanza kutengeneza utaratibu wa namna ambayo tunadhibiti soko kwa maana ya ya kuangalia jinsi ambavyo tutasajili bidhaa za tumbaku,” anasema.


Fimbo anasema Sheria inataka kutengwa maeneo kwa ajili ya uvutaji sigara kama vile kwenye kumbi za starehe, mabaa, mikusanyiko ya watu mahotelini na kadhalika.


Anasema kuwa mamlaka hiyo ina kazi kubwa ya kutoa elimu kwa jamii namna sahihi ya kuvuta sigara, ikiwemo mazingira na athari za bidhaa hizo.


“Tuko kwenye utaratibu wa kuweka mfumo mzuri wa matumizi wa bidhaa za tumbaku,” anasema.


Sigara inaua kuliko ajali

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi, aliwahi kukaririwa na gazeti hili akisema: “Ukiuliza watu mjini ni nini kinaua zaidi kati ya bodaboda au sigara, kila mmoja atakuambia ni bodaboda. Hapana!”


Akaongeza:  “Duniani, sigara inaua watu wengi zaidi kuliko ajali, pombe na virusi vya ukimwi. Ukijulimsha hizi sababu zote, sigara ndiyo inaua zaidi… Maanake ukichukua ajali, bia, HIV, wanaojiua, vifo vya nyumbani na dawa za kulevya, sigara inakuwa na vifo vingi zaidi.”


Dk Janabi alilinganisha vifo vya sigara na ajali za pikipiki kuonesha ukubwa wa tatizo tofauti na mtazamo wa jamii ulivyo.


Alisema sigara ni kitu ambacho kikitazamwa haraka, inawezekana ikachukuliwa kuwa nchi inapata faida. “Lakini ukitazama kwa muda mrefu, hiyo faida ndiyo inakuja kutumika kwenye kutibu wanaoathirika na tumbaku.”


Dk Janabi alisema moja ya tano ya wagonjwa wanaowafanyia tiba ya moyo tatizo lao la moyo limetokana na sigara na kwamba wengi wa wagonjwa hao wanakwenda kwenye taasisi hiyo kwa sababu ya mishipa ya damu kuharibika.


Alifafanua kwamba mishipa inaweza ikawa imeharibika kwa sababu ya mafuta (cholesterol) au kwa sababu ya sigara na kwamba wanapozungumza na wagonjwa hao, moja ya tano miongoni mwao hukiri kuwa waliwahi au wanaendelea kuvuta sigara.


“Endapo serikali ingewapeleka nje ya nchi kwa kipindi hicho (tulichokuwa hatuna hii ya taasisi), mgonjwa mmoja alikuwa aki gharama ya Sh milioni 30 India. Unaweza kuangalia athari yake katika uchumi. Kwa hiyo faida yote uliyotengeneza kutokana na zao la tumbaku, sasa unakwenda kuitumia kwenye matibabu,” anasema.


Kwa hapa nchini, alisema gharama za matibabu si chini ya Sh milioni sita na kwa takwimu za dunia, uvutaji wa sigara katika Afrika unazidi kwenda juu. “Tumetoka kwenye kuvuta sigara 700 kwa mwaka hadi 1,200 kwa mwaka na ukitazama Tanzania, wanaume ndiyo wavuta sigara zaidi.”


Gharama ya matibabu kwa mishipa iliyoziba kwa maana ya kufanyiwa upasuaji alisema ni Sh milioni 29. Profesa Janabi alihimiza wadau ikiwamo vyombo vya habari kupiga kampeni dhidi ya matumizi ya bidhaa zote za tumbaku.


Alisema licha ya kuharibu moyo, tumbaku huchangia saratani ya njia ya chakula, ya koo, mapafu na ugonjwa ambao hautibiki ujulikanao kama COPD.


“Hizi athari siyo za kutunga… Binafsi sijawahi kuvuta sigara katika maisha yangu lakini natibu wagonjwa ambao wameathirika na sigara, kwa hiyo naona shida wanazozipata,” alisisitiza.


Kuhusu watoto, Profesa Janabi alisema: “Kumekuwa na watoto wetu wengi wanaonekana kama wana pumu… hao second smokers (wanaovuta moshi wa wavutaji wengine) baba anavuta, jirani anavuta na unakwenda kuwaathiri.”


Gazeti hili pia liliwahi kumkariri Daktari Bingwa wa magonjwa ya watoto, Dk Francis Kuria akikiri kuwapo watoto wengi wanaofikishwa hospitalini wakiwa na pumu ambapo hubainika badaye kwamba wamevutishwa moshi na wavutaji sigara.


Dk Kuria kutoka Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Watoto Tanzania (PAT) alisema mtu anapovuta sigara ndani ya gari au nyumbani na baadaye watoto wakaingia, mabaki yake yana athari kwao. Vivyo hivyo kwa mtoto anayekaa karibu na mtu anayevuta sigara.


Dk Johnson Katanga kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Kitengo cha Kinga, naye aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba takribani asilimia 32 ya wagonjwa wanaowapokea, husumbuliwa na maradhi ambayo huhusishwa na uvutaji wa sigara.


Daktari huyo alisema moshi wa sigara umehusishwa na saratani nyingi huku ya mapafu ikitajwa moja kwa moja kutokana na uvutaji sigara au matumizi ya bidhaa zingine za tumbaku.


 “Kwa sasa duniani, saratani inayoongoza duniani ni ya mapafu na kisababishi kikuu ni uvutaji wa sigara au tumbaku,” alisisitiza. Saratani nyingine zinazohusishwa na tumbaku ni ya koromeo, mdomo, koo, tumbo, utumbo mpana na shingo ya kizazi.


Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2003 zinaonesha kuwa kila baada ya sekunde 10, mtu mmoja hufariki dunia kutokana na maradhi yanayotokana na matumizi ya bidhaa za tumbaku.


Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2025, vifo vinavyotokana na matumizi ya tumbaku vitaongezeka kwa asilimia 70. Aidha, ifikapo  mwaka 2030, watu milioni 10 watakufa kila mwaka kutokana na uvutaji wa sigara duniani.


Kulingana ya WHO, asilimia 70 ya wavutaji wanatoka katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania. Wanaume wanaovuta sigara Afrika ni asilimia 36 na wanawake ni asilimia tisa.


Mwandishi Isdory J. Mushi, katika kitabu: “Pombe, Sigara na Dawa za Kulevya: Madhara Kiafya, Kiroho, Kijamii na Ukimwi” cha Novemba 2005, anasema: “Wenzio wanakuuzia sigara, lakini wamekwishajihami kisheria. Hata sigara yao ikikudhuru, hutaweza kuwashitaki na kulipwa fidia yako. Napenda Mungu afumbue ufahamu wa wavuta sigara, ili waweze kuona unafiki wa shetani.”


Alisema kimsingi neno, ONYO, kwenye paketi ya sigara linawakilisha madhara na hatari nyingi dhidi ya maisha ya mtumiaji wa moja kwa moja, na watumiaji wasio wa moja kwa moja yaani, wanaovutishwa bila wao kutaka au kujua na hao, wanaathirika zaidi.


Alisema ingawa sigara ni wakala mkubwa wa magonjwa yasiyoambukiza (NCD), katika kitabu hicho, Mushi anakwenda mbali na kusema, baadhi ya magonjwa ya mdomoni huambukizwa kwa sigara.


Anaandika: “Wavuta sigara wasio na kipato kizuri, wanakuwa hatarini kupatwa na magonjwa mengine, mfano kipindupindu, Ukimwi, kifua kikuu n.k. kwa sababu ya kuomba ‘pafu’ au sigara iliyovutwa na mtu aliyeathirika na magonjwa hayo…”


Sheria kudhibiti uvutaji holela

Sheria ya kudhibiti bidhaa za tumbaku ya mwaka 2003 ililenga kuhakikisha watu hawapati madhara makubwa yanayotokana na moshi wa sigara au tumbaku kutokana na wavutaji kwenye mikusanyiko ya watu.


Sheria hiyo inawataka wananchi wanaotumia bidhaa za tumbaku, kupunguza au kuacha kabisa. Pia inajumuisha jamii yote kujua madhara ya matumizi ya tumbaku na umuhimu wa kuzuia uvutaji katika maeneo ya umma.


Licha ya kuwepo kwa sheria hiyo, utekelezaji wake kwa vitendo kwa muda mrefu umekuwa hauonekani dhahiri. Ni jambo la kawaida kushuhudia wanaovuta sigara katika mkusanyiko wa watu wakiwa hawana wasiwasi kwa vile hakuna wanaokamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuvunja sheria hiyo ya nchi.


Suluhisho

Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania (TTCF) kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wake, Lutgard Kagaruki anashauri serikali na wadau kuhimiza mazao mbadala wa tumbaku.


Watu mbalimbali wanapendekeza kodi katika bidhaa za tumbaku iongezwe maradufu ili watumiaji wapungue kwa kushindwa kumudu.


Ingawa ni vigumu kuunda sheria kubana watu kuvuta sigara nyumbani, WHO inasema ipo haja ya hatua kuchukuliwa kulinda watoto kutokana na madhara ya moshi wa sigara.


Wengine wanasema uwepo mjadala wa kitaifa kuona kama bado kuna haja ya kujikita katika kilimo na uzalishaji wa tumbaku na bidhaa zake, au jamii ijikite katika mazao na bidhaa mbadala zisizo na madhara kwa jamii.

Post a Comment

0 Comments