Ticker

6/recent/ticker-posts

 


Hukumu ya Aveva na Kaburu sasa ni Oktoba 28

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara nyingine tena imeahirisha kusoma hukumu ya aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange 'Kaburu' kwa sababu  Hakimu bado hajamaliza kuiandaa.

Hukumu hiyo ambayo ilipaswa kusomwa na Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba leo inaahirishwa kwa mara ya pili ambapo awalo ilikuwa isomwe Oktoba 6,2021 lakini ikaahirishwa hadi leo Oktoba 21 na sasa imeahirishwa hadi Oktoba 28,2021.

Mapema kesi hiyo ilitwa mbele ya Hakimu Simba majira ya saa tano asubuhi lakini ikaahirishwa hadi saa nane mchana ambapo pia imeahirishwa. 

Aveva na Kaburu walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Juni 29, 2017 na kusomewa mashtaka kumi ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka, kula njama na kughushi nyaraka zilizoonesha kuwa klabu hiyo ilikuwa ikililipa mkopo wa dola za Marekani 300,000 kwenye akaunti ya Aveva na utakatishaji haramu wa fedha.

Kesi hiyo iliendelea kutajwa washtakiwa hao wakiwa mahabusu hadi ilipofika Septemba 19, 2019 walipoandika barua ya kukiri na kuomba kumaliza kesi hiyo kwa njia ya majadiliano na Mkurugenzi wa mashtaka (DPP) lakini upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa walikuwa katika mchakato wa kuwafutia mashtaka ya utakatishaji fedha washtakiwa hao na ikalazimu majadiliano hayo kusubiri, hata hivyo hayakufanyika.

Oktoba 11, 2019 washtakiwa hao walifutiwa mashtaka ya utakatishaji fedha haramu na kupewa dhamana 

Katika kesi hiyo inadaiwa,  Aveva na Kaburu walikula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka na pia walidaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha USD 300,000 kutoka kwenye akaunti ya klabu ya Simba iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.

Katika shtaka la tatu, Aveva walidaiwa kwa pamoja kughushi nyaraka zilizoonesha kuwa Simba ilikuwa inalipa mkopo wa kiasi hicho cha fedha kwa Aveva jambo ambalo walijua kuwa si kweli.

Pia Aveva anadaiwa kutoa nyaraka za uongo kwa benki ya CRDB akionesha klabu ya ya Simba wanalipa mkopo huo.

Aveva anadaiwa kuwa katika Benki ya Baclays Mikocheni alijipatia USD 187,817 wakati akijua zimetokana na kosa la kughushi nyaraka.

Katika shtaka la sita, Kaburu alidaiwa kumsaidia Aveva kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwenye akaunti klabu ya Simba wakiwa wanajua fedha hizo zimetokana na kughushi nyaraka.

Pia walidaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionesha kwamba klabu ya Simba ilinunua nyasi bandia kwa gharama ya dola za Marekani 40,577 huku wakijua kwamba siyo kweli.

Katika shtaka la nane, Aveva anadaiwa kuwasilisha hati ya malipo ya kibiashara ya uongo  kwa Levison Kasulwa  kwa madhumuni ya kuonesha kwamba Simba wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya USD 40,577 huku shtaka la tisa ilidaiwa washtakiwa hao waliwasilisha nyaraka za uongo kuonesha kuwa Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya dola za Marekani 40,577.


 

Post a Comment

0 Comments