Mfanyabiashara nguli wa dawa za kulevya akamatwa Colombia

 


Mfanyabiashara wa mashuhuri wa dawa za kulevya na kiongozi wa genge kubwa la uhalifu aliyekuwa akisakwa huko nchini Colombia amekamatwa.


Dairo Antonio Úsuga, anayejulikana kama Otoniel, alikamatwa baada ya operesheni ya pamoja ya jeshi, jeshi la anga na polisi siku ya Jumamosi.


Serikali ilikuwa imetoa zawadi nono ya $ 800,000 (£ 582,000) kwa yoyote ambaye anafahamu mahali alipo, huku Marekani ikiweka dau la dola milioni 5.


Rais Iván Duque alipongeza kukamatwa kwa Otoniel katika ujumbe wa video uliorushwa kwenye runinga ya Taifa.


"Huu ni ushindi mkubwa dhidi ya biashara ya dawa za kulevya katika nchi yetu kwenye karne hii," alisema. " Ushindi huu unafananishwa tu na anguko la Pablo Escobar miaka ya 1990."


Otoniel alikamatwa katika maficho kwneye vijiji vya mkoa wa Antioquia kaskazini magharibi mwa Colombia, karibu na mpaka na Panama. Wakati maelezo ya operesheni bado yakiibuka, rais alisema afisa mmoja wa polisi aliuwawa kwenye majibizano ya risasi.


Wanajeshi wa Colombia walitoa picha inayoonyesha wanajeshi wake wakimzingira Otoniel aliyefungwa pingu.


Otoniel alikuwa kiongozi wa ngazi za juu katika kundi la Gulf ambalo kwasasa linaitwa Usaga, kiongozi wa awali ambaye alikuwa kaka yake mkubwa aliuliwa na polisi katika sherehe za kukaribisha mwaka mpya miaka kumi iliyopita.


Jeshi la Ulinzi nchini Colombia limeweka kundi hilo kama moja ya kundi lenye nguvu la uhalifu huku Marekani ikiangazia kwa kusema kuwa kundi hili limekuwa linamiliki silaha nzito za kivita.


Genge la kihalifu, ambalo linafanya kazi katika majimbo mengi na lina uhusiano mkubwa wa kimataifa, linajishughulisha na biashara ya dawa za kulevya na uuzaji wa binadamu pamoja na uchimbaji haramu wa dhahabu.


Inaaminika kuwa na wanachama wapatao 1,800 wenye silaha ambao huajiriwa kutoka kwa vikundi vya wanamgambo. Wanachama hao wengi wao wamekamatwa huko Argentina, Brazil, Honduras, Peru na Uhispania.


Inaaminika kuwa Genge hilo linadhibiti njia nyingi zinazotumika kusafirisha dawa za kulevya kutoka Kolombia kwenda Marekani hadi Urusi.


Serikali ya Colombia, hata hivyo, iinayo matumaini kwamba imepunguza idadi kubwa ya wanachama wa kundi hilo pamoja na magenge mbalimbali ya kiuhalifu ndani ya miaka ya hivi karibuni, na kulazimisha wanachama wengi wanaoongoza kujificha katika maeneo ya mbali kwenye msitu.


Otoniel sasa anakabiliwa na mashtaka kadhaa ikiwa ni pamoja na kupeleka shehena ya kokeni Marekani, kuua maafisa wa polisi na kuajiri watoto.


Alishtakiwa nchini Marekani tokea mwaka 2009, na sasa ni ataanza mchakato wa kupelekwa New York kusomewa mashataka zaidi.

Post a Comment

0 Comments