Rais Samia aipongeza wizara ya afya kwa kufanikiwa kupambana na corona


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Sukuhu hassan ameipongeza Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kwa kufanikiwa kubuni mbinu za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya uviko 19 kwa kueneza elimu kwa wananchi mijini na vijijini ambapo takwimu zinaonyesha watu 846,000 wamepatiwa chanjo ya Corona.

Mhe. Samia Suluhu Hassan amebainisha hayo katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma mara baada ya kuzindua rasmi kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19

Mhe.Samia Suluma Hassan amesema Katika kipindi cha miezi sita serikali imefanyia kazi huduma zinazogusa wananchi moja kwa moja, kupitia Wizara ya Afya na kufanikiwa kupambana na maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) kwa kufanikisha upatikanaji wa dozi 1,518,400 kutoka serikali ya watu wa marekani.

Mhe Rais amesema hivi karibuni serikali imepokea dozi nyingine 1,0565,000 kutoka taasisi ya COVAX Facility ambapo takwimu zinaonyesha kufikia oktoba 9 mwaka huu jumla ya wananchi imefikia 846,000 huku hamasa na kampeni zikiendelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Amesema, serikali kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kujenga kiwanda cha kutengeneza vifaa vya kujikinga na maradhi ya UVIKO-19 ikiwemo barakoa na vifaa vingine jijini Dar es salaam na imetumia shilingi bilioni 234 kununua dawa na Shilingi bilioni 26.3 kununua vifaa tiba mbalimbali  ikiwemo Digital x-ray, CT-SCAN na ultrasound.

Mhe.Rais Samia amesema serikali imetumia shilingi bilioni 7.9 kununua mashine ya kupasulia ubongo bila kufungua kichwa katika Taasisi ya Mifupa ya Moi huku serikali ikitumia Shilingi bilioni 159 kuendeleza ujenzi wa miradi 25 ya hospitali za rufaa, mikoa na kanda.

“Vilevile kupitia tozo ya miamala za simu serikali imetoa bilioni 37.5 kujenga vituo vya afya katika tarafa 150 kati ya tarafa 207 ambazo hazina vituo vya afya,” ameongeza Rais Samia.

Awali Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba amesema kwa upande wa sekta ya afya, serikali imetenga bilioni 469.9 kuboresha huduma ya afya ikiwemo kujenga ICU katika kila hospitali ya rufaa maalumu za mikoa na baadhi ya wilaya kuongeza ICU 72 kutoka ICU 75 zilizokuwepo.

“Hii ni kwa ajili ya adha iliyokuwa inajitokeza mgonjwa anapokuwa amefikia hatua ya kuwekwa ICU kama anatokea katika eneo ambalo hakuna huduma angalizi ya aina hiyo maana yake uwezekano wa kunusuru maisha yake unakuwa mdogo.

Amesema serikali inaendelea kununua vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya ICU  72 zinazoenda kuongezeka na tayari pesa imeshatengwa takribani shilingi bilioni  54 na kwamba kuna ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za dharura za kisasa zenye EMDs katika hospitali ya taifa, hospitali za rufaa, mikoa na baadhi ya wilaya.

Dk Mwigulu amesema jumla ya hospitali 105 zinaenda kuongezeka kutoka hospitali 10 zilizokuwa na mundombinu ya aina hiyo sambamba na kuongeza upatikanaji wa magari ya wagonjwa (ambulances)  ambapo serikali imepanga kuongeza jumla ya magari 20 ya kisasa ya kubebea wagonjwa.

“Hapo awali zilikuwepo mbili tu na tunaenda kuongeza ambulances za kawaida ambazo zitaenda kwenye halmashauri zetu 375 kwa wastani wa kila halmashauri na magari ya kutolea chanjo 214 ili huduma hiyo iendelee kufanya vizuri,” amesema Dk Mwigulu.

Post a Comment

0 Comments