Ticker

6/recent/ticker-posts

Vitambue vitu muhimu ndani ya chumba cha kulala

 Leo tumekuja kivingine ambapo tunaangalia vitu saba vinavyohitajika na ni muhimu kwenye chumba cha kulala.

Hakuna asiyependa kulala sehemu nzuri na kwanza ukilala sehemu nzuri, kuna faida yake ikiwa ni pamoja na kukupunguzia mawazo, uchovu na mambo mengine mengi.

Wapo ambao wanatamani kulala sehemu nzuri, lakini hawajui wafanyeje, hivyo kwa kupitia ukurasa huu, wanaweza kupata wanachokihitaji kujua na kuweza kufikia kile wanachokitamani kwa muda mrefu. Karibu ungana nami hapa chini:

KITANDA NA MATANDIKO

Ukweli ni kwamba, kitanda na matandiko ni vitu muhimu, kwani ndivyo vimesababisha chumba hiki kiitwe chumba cha kulala.

ZULIA

Hakikisha kwenye chumba chako unaweka zulia ambalo siyo lile la manyoya hata kama siyo chumba kizima, basi weka hata lile dogo la pembeni mwa kitanda ili ukiamka asubuhi hatua yako ya kwanza iwe ya burudani kuliko kukanyaga kwenye sakafu ambayo ina baridi itakayokufanya usione raha.

MITO YA KUTOSHA

Unaangalia ukubwa wa kitanda chako ambapo idadi sahihi ya mito ni kuanzia miwili hadi sita. Kitanda kiwe na mito ya kulalia pamoja na ile ya mapambo. Pia muundo wa mito ya mapambo unaweza kuwa wowote kama vile pembe nne, soseji na moyo. Kwa kulalia, mito inayofaa ni ile ya pembe nne.

ENEO LA KUKAA

Eneo la kukaa ambalo siyo kitandani, linakusaidia wakati wa kusoma au wa mazungumzo na mwenzi wako. Pia ni pazuri kunyanyulia mguu wakati wa kuvaa soksi. Vilevile unapotaka kulala unahitaji kuondoa na kuhifadhi vile vitu ulivyopambia kitanda kama vile mito, utepe wa kitanda na shuka au duveti la mapambo kwenye eneo hilo la kukalia kwa ajili ya kuvitandika siku inayofuata.

Kama kuna baridi, unaweza kutumia duveti kujifunika.

VITU NA PICHA UNAZOZIPENDA

Chumba hakitakiwi kuwa na mrundikano wa vitu vingi au mapicha mengi, ila unaweka vitu vichache unavyovipenda eneo unaloviona kwa muda mrefu na vitu hivyo vinazidisha furaha yako. Unapokuwa na furaha, unapata usingizi mzuri na unapoamka unaanza siku kwa furaha.

TAA ZA VIVULI KILA UPANDE WA KITANDA

Wakati mwingine ukiwa umelala unajisikia kusoma kitabu, jarida au gazeti. Ili usimsumbue wa pembeni yako kwa mwanga, tumia taa ya kivuli iliyo upande wako ndiyo suluhisho. Zaidi taa hizi ni sehemu ya kupendezesha chumba.

PAZIA

Chumba cha kulala kinahitaji faragha na hisia za giza hata kiwe ni cha rangi za mwanga kiasi gani. Weka pazia sahihi.

Usikifanye chumba cha kulala kama jikoni, hivyo tafuta mapazia ambayo siyo ya kung’aa yanayoendana na rangi ya kitanda au mashuka unayotandika.

NYONGEZA

Pamoja na vitu hivyo saba, kama chumba chako ni kikubwa, unaweza kuweka pia dressing table kama unapenda.

Post a Comment

0 Comments