Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amezindua nyumba za maafa kwa Wananchi waliokumbwa na mafuriko mwaka 2017 huku akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za makusudi kuzuia na kupunguza madhara yanapotokea majanga.
Hafla hiyo imefanyika leo Jumanne Novemba 23, 2021 katika kijiji cha Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo jumla ya nyumba 15 zimezinduliwa.
Dk Mwinyi amesema miongoni mwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa ni kuendeleza mipango miji ambayo inabainisha sehemu za ujenzi wa makaazi, sehemu za mabonde zisizopaswa kujengwa, maeneo ya kilimo, maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na maeneo ya huduma za jamii.
“Ni vyema tukahakikisha tunakuwa na master plan (mpango kabambe) ya kila mji tunaoujenga ili kuweka mifumo na taratibu nzuri za kupambana na maafa,” amesema Dk Mwinyi.
Amesema majanga na maafa yamekuwa yakijitokea katika nchi zote duniani kwa namna mbalimbali, hata hivyo hakuna teknolojia ambayo imetengenezwa kuzuia majanga na maafa yasitokee.
Naye Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dk Saada Mkuya amesema jumla ya familia 54 ambazo zinaidadi ya watu 291 kwa Unguja na Pemba wanaishi katika vijiji hivyo ambapo wanafunzi wa Maandalizi na Msingi 277, wanasoma katika vijiji hivyo kat yao 151 Nungwi na 126 Tumbe.
Kwa upande wa vituo vya afya tangu vifunguliwe tayari wananchi 954 wamepatiwa matibabu na huduma mbalimbali za kiafya wakiwemo 230 Tumbe na 724 Nungwi.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Thabit Idarous Faina amesema ujenzi wa nyumba hizo unatokana na athari za mvua za masika zilizonyesha mwaka 2017 ambapo nyumba 6005 ziliathirika Unguja na Pemba.
Mmoja wa wanufaika na nyumba hizo, Amina Juma amesema “tunaishukuru serikali kwasbabu wengine hatukuwa na uwezo wa kujenga baada ya mali zetu kuharibiwa lakini kwasasa tunaishi tena zaiid ya ilivyokuwa awali.”
Nyumba 15, kituo cha afya, shule, maabara, msikiti na maduka 15 vyote vimejengwa katika vijiji vya Nungwi na Tumbe kisiwani Pemba.
Nyumba hizo zimejengwa na seriklai ya Mpainduzi kwa kusaidiana na taasisi ya Mwezi Mwekundu kutoka Falme za Kiarabu (UAE) ambapo pamoja na nyumba za kuishi pia kuna kituo cha afya, shule, maabara, msikiti na maduka 15.