Nov 24, 2021

LHRC yalaani Polisi kumpiga, kumjeruhi kijana Goba

  Muungwana Blog       Nov 24, 2021


Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani kitendo cha polisi kituo cha Goba kumpiga na kumjeruhi kijana Issa Kassimu (22) na kusababishwa kulazwa chumba maalumu cha uangalizi (ICU).


Inadaiwa kuwa Kassimu alijeruhiwa na askari hao Novemba 10, 2021 baada ya kukamatwa kwa tuhuma za wizi wa runinga na baadae kupigwa huku ndugu zake walikuwa wakiombwa rushwa ili aachiwe.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 24, 2021 Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema wamepokea taarifa kuwa Kassimu ambaye kwasasa yuko katika chumba maalumu cha uangalizi (ICU) katika Hospitali ya Muhimbili bado hali yake sio nzuri.


“Kwa hali ya kawaida Watanzania wangependa kuona Jeshi la Polisi likishirikiana na ndugu wa mgonjwa ili kupata ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani askari hao. Tumepata taarifa mmoja wa ndugu aliitwa Kituo cha Polisi Oysterbay alipekuliwa kama mhalifu na kunyang’anywa simu zake mbili,” amesema.


Amesema vitendo vya askari polisi kuwashambulia na hata kupelekea vifo vya watuhumiwa vimekuwa vikitokea mara kwa mara hivyo endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa maaskari wachache watalichafua jeshi hilo.


Ametoa wito kwa jeshi hilo, kuhakikisha ndugu wa mhanga hawanyanyaswi na wanapata taarifa sahihi za hatua zilizochukuliwa dhidi ya askari wanaotuhumiwa.


“Pia kuhakikisha kwamba Serikali inaunda timu ya kuchunguza tukio hilo na kupata ushahidi hasa kutoka kwa madaktari waliompokea na kumtibu kijana ambao wako tayari kutoa ushirikiano. Jeshi haliwezi kujichunguza lenyewe,” amesema.


Akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai amesema upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea.


“Hilo suala alikwishalizungumzia Kamanda Muliro kwasababu sisi hatufanyi kazi kwa kuangalia kwenye mitandao ya kijamii. Kuhusu kuchukuliwa simu amechukuliwa kwaajili ya uchunguzi kama inadaiwa huyu askari wetu kaomba pesa na mazungumzo yalifanyika kwa njia ya simu ya mtuhumiwa na huyo aliyepigiwa simu, kwahiyo tunachukua simu kufanya uchunguzi.


“Sasa tena tunachukua simu kwaajili ya uchunguzi mnasema kanyang’anywa, zimechukuliwa kama sehemu ya kielelezo kwaajili ya uchunguzi. Lakini hilo suala la kupigwa uchunguzi unaendelea na kuhusu vitisho sijui ila hilo ni kosa la jinai yeyote anayetishwa akaripoti kituo cha polisi,”amesema Kingai.

logoblog

Thanks for reading LHRC yalaani Polisi kumpiga, kumjeruhi kijana Goba

Previous
« Prev Post

No comments:

Post a Comment