Kansela wa Ujerumani anayeondoka Angela Merkel na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg wameelezea wasiwasi kuhusu mzozo kwenye mpaka kati ya Belarus na Poland, na ule wa kati ya Urusi na Ukraine.
Viongozi hao wanafanya mazungumzo mjini Berlin ambapo wote wawili wamesema hali inayoendelea mpakani hapo ni ya kutia wasiwasi.
Kabla ya mazungumzo na mkuu huyo wa NATO, Merkel alisema wakati wote yeye aliunga mkono mazungumzo kati ya Urusi na muungano huo wa kijeshi wa nchi magharibi. Lakini bahati mbaya hakujawa na hali ya utulivu iliyoshuhudiwa kwa sasa.
Stoltenberg amesema NATO inahititaji Ujerumani iliyo imara kisiasa na kijeshi. Maafisa nchini Poland wamesema leo kuwa hakuna wahamiaji wanaoendelea kupiga kambi kwenye upande wa Belarus wa mpaka wa mashariki mwa Umoja wa Ulaya, lakini majaribio ya kutaka kuvuka kwa nguvu kuingia katika umoja huo yanaendelea.