Uingereza kuorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi


Serikali ya Uingereza inapanga kuorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi. Hii ina maana kuwa yeyote atakayeonyesha uungwaji mkono kwa kundi hilo nchini Uingereza huenda akaadhibiwa na kifungo cha miaka 14 jela. 


Waziri wa Mambo ya Ndani Priti Patel amesema atashinikiza mabadiliko hayo bungeni wiki ijayo, akilenga kuiweka Uingereza kwenye njia sawa na Marekani, ambayo ililiorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi mwaka wa 1995, na Umoja wa Ulaya. 


Patel anahoji kuwa hatua ya kupiga marufuku ya moja kwa moja chini ya Sheria ya Ugaidi ya 2000 ni muhimu kwa sababu sio rahisi kutenganisha kati ya tawi la kisiasa la Hamas na la kijeshi. 


Tawi la kijeshi la al-Qassam Brigades la vuguvugu hilo la linalotawala Ukanda wa Gaza limepigwa marufuku Uingereza tangu Machi 2001. Patel ambaye yuko ziarani Marekani, amesema kundi hilo linaendesha chuki dhidi ya Wayahudi na linapaswa kupigwa marufuku ili kuwalinda Wayahudi.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi