Serikali ya Tanzania yaagiza kuanzishwa madawati kijinsia katika shule za msingi na Sekondari

 


Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema serikali itaendeleza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na haitavumilia aina yoyote ya ukatili wa kijinsia utakaofanywa na yeyote.


Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.


Majaliwa amesema nguvu kubwa inatakiwa kuongezwa katika kukabiliana na tatizo hilo linaloathiri vijana wengi wa kike.


“Lazima jamii yetu ijenge msukumo wa kuhakikisha kuwa kila mtu katika nafasi yake anapaza sauti na kuchukua hatua ya kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani ukatili wa kingono kama vile rushwa ya ngono, ukatili baina ya wenza, ubakaji, mimba na ndoa za utotoni”.


Majaliwa ameiagiza Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuandaa mpango mpya; Kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa za ukatili katika ngazi zote; kusimamia utekelezaji wa sera na sheria hususan Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, pamoja na kusimamia uendeshaji wa usimamizi wa Mahakama ya Familia ili kuimarisha ushughulikiaji wa migogoro ya ndoa na familia.

Post a Comment

0 Comments