Sudan imeanzisha uchunguzi kuhusu ukiukaji wa haki dhidi ya waandamanaji tangu mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 25, Waziri Mkuu aliyerejeshwa madarakani Abdalla Hamdok amesema.
Bw Hamdok alisema hayo Jumanne baada ya kukutana na wanachama wa Forces of Freedom and Change (FFC), muungano wa zamani wa kiraia unaotawala ambao umekuwa ukipinga utawala wa kijeshi.
Shirika la Habari la Sudan (Suna) linalomilikiwa na serikali liliripoti kwamba muungano huo sasa unaunga mkono mpango wa Bw Hamdok na wanajeshi baada ya mazungumzo ya mjini Khartoum.
Muungano huo hapo awali ulikuwa umesema hautambui makubaliano yoyote ya kisiasa na uongozi wa kijeshi kufuatia kurejeshwa kwa Bw Hamdok.
Siku ya Jumanne, Waziri Mkuu na kundi hilo walitaka wafungwa wa kisiasa waachiliwe na jeshi liheshimu haki za kufanya maandamano ya amani.
Udhibiti wa jeshi mwezi uliopita ulisababisha maandamano, na zaidi ya watu 40 wameripotiwa kuuawa wakati wa maandamano.