Ticker

6/recent/ticker-posts

 


Waliovamia vyanzo vya maji Kilimanjaro kuchuliwa hatua


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Said Mtanda kuchukua hatua za haraka kuwadhibiti  watu waliovamia eneo lenye  chanzo cha maji Njoro ,kata ya Miembeni wilayani humo.


Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu huyo wa mkoa kupata taarifa kutoka kwa diwani wa kata hiyo, Mohamed Mushi kuwapo baadhi ya watu wanauza viwanja Sh5 milioni eneo karibu na chanzo hicho cha maji.


Akizungumza mara baada ya kufika katika chanzo hicho cha maji amesema hatakubali kuvumilia wala kuona vyanzo vya maji vikiharibiwa na kuhujumiwa na watu wachache ambao wana nia ovu ya kudhulumu mali za Serikali ambapo ameagiza wachunguzwe na kuchukuliwa hatua.


"Mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa Muwsa naagiza  haya maeneo lazima tuyalinde maana hii changamoto ya maji tunayoipitia sasa hivi ni kwasababu maeneo mengi tumeyaachia tuu,haya maeneo ya vyanzo vya maji lazima tuwe nayo makini," amesema Kagaigai


"Kwa haraka sana chochote kinachofanyika hapa naomba kusimame, ikiwezekana RPC tumieni polisi kuwaondoa wavamizi kwenye hivi vyanzo ili tuhakikishe tunalinda haya maeneo vinginevyo tutapata shida ,na mimi siwezi kukubali,"


Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Said Mtanda amemhakikishia Mkuu huyo wa mkoa kuchukua hatua za haraka ikiwemo kusimamisha shughuli zote zilizokuwa zikifanywa kando kando ya chanzo hicho cha maji ikiwemo uuzaji wa viwanja.


"Mheshimiwa Mkuu wa mkoa tutachukua hatua za haraka na tutamtafuta anayegawa hii ardhi na kuanzia sasa nimesitisha zoezi hilo mpaka tathmini ifanyike kujua huyu anayesema hili eneo  alilipata kwa uhalali gani ,"amesema na kuongeza


"Nitaunda kamati ndogo nitashirikisha watu wa ardhi,mamlaka ya maji (Muwsa ),bonde la pangani na nitakuletea ripoti ,endapo tukiona wamekiuka sheria tutawafikisha kwenye vyombo vya sheria,"amesema Dc Mtanda

Post a Comment

0 Comments