Rais wa China Xi Jinping amesema nchi yake haitatafuta udhibiti wa kanda ya Kusini mashariki mwa Asia au kuwadhulumu majirani zake wadogo, wakati kukiwa na mgogoro unaoendelea kuhusu umiliki wa Bahari ya Kusini mwa China.
Xi ametoa kauli hiuo wakati wa mkutano wa video na wanachama wa Jumuiya ya Kusini Mashariki mwa Asia - ASEAN, ulioandaliwa kuadhimisha miaka 30 ya mahusiano kati ya China na kundi hilo.
Xi amesema China inapinga vikali siasa za ubabe, na ingependa kudumisha mahusiano wa kirafiki na jirani zake na kutafuta amani ya kudumu katika kanda hiyo.
Myanmar haikuwakilishwa katika mkutano huo wa leo baada ya serikali yake iliyowekwa na jeshi kukataa kumruhusu mjumbe wa ASEAN kukutana na kiongozi aliyeondolewa madarakani Aun San Suu Kyi na wanasiasa wengine waliokamatwa.
Mtawala wa kijeshi Jenerali Min Aung Hlaing pia alizuiwa kuiwakilisha nchi yake katika mkutano wa kilele uliopita.