Rais Cyril Ramaphosa amewataka wanaume wa Afrika Kusini kuchukua jukumu kubwa katika kuzuia unyanyasaji wa kijinsia (GBV) nchini humo.
"Iwapo kila mwanamume atakusanya wanaume wawili na watatu kuahidi kutowahi kumbaka mwanamke, kamwe kumnyooshea mkono mwanamke na kuwajibishana kwa ahadi hii, tunaweza kuanza kukabiliana na ukatili wa kijinsia nchini mwetu," Bw Ramaphosa. aliandika kwenye barua yake kwa Waafrika Kusini.
Aliongeza kwamba ukatili dhidi ya wanawake ni janga na wanaume ndio wa kulaumiwa zaidi.
"Wanaume wengi ndio hufanya ubakaji. Hasa wanaume ndio wahusika wa unyanyasaji wa nyumbani."
Maoni ya Bw Ramaphosa yanafuatia kutolewa kwa takwimu za hivi punde zaidi za uhalifu na polisi, ambazo zinaonyesha ongezeko la visa vya ubakaji, unyanyasaji wa nyumbani na mauaji ya watoto.
Kati ya Julai na Septemba mwaka huu, watu 9,556, wengi wao wakiwa wanawake, walibakwa. Hili ni ongezeko la 7% kutoka kipindi cha awali cha kuripoti.
Rais aliwataka Waafrika Kusini kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha kuwa siku 16 za mwaka huu za uharakati dhidi ya GBV, ambazo zitaanza Alhamisi, "zina maana" na "zinapita zaidi ya maneno tu".