Austria imeanza rasmi kutekeleza amri ya kuzuwia baadhi ya shughuli muhimu za maisha ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya wimbi la nne la maambukizo ya virusi vya corona.
Hatua hiyo inakuja wakati idadi ya wastani ya vifo kwa siku ikiongezeka mara tatu zaidi katika wiki za karibuni na baadhi ya hospitali zikionya kuwa vyumba vyao vya wagonjwa mahututi vinaelekea kujaa.
Zuio la sasa limepangwa kuwapo kwa siku 10, lakini upo uwezekano wa kuongezwa hadi 20, ambapo watu wanaruhusiwa tu kutoka majumbani mwao wakiwa na sababu za msingi, kama vile kununuwa vyakula, kumuona daktari ama kufanya mazoezi.
Hapo jana miji kadhaa ya Ulaya ilishuhudia maandamano ya maelfu ya watu wanaopinga hatua nyengine za kuufunga uchumi na shughuli nyengine kujikinga na COVID-19.