Kenya imegundua visa vitatu vya kwanza vya aina mpya ya virusi vya Covid 19 , Omicron vilivyogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini mwezi uliopita.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema visa hivyo viligunduliwa miongoni mwa wasafiri.
Wiki iliyopita, Uganda ilitangaza kuwa imegundua visa vya Omicron kwa wasafiri wanaokuja nchini, maambukizi ya kwanza kuripotiwa Afrika Mashariki.
Visa hivyo viligunduliwa kwa watu waliopimwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe ambao walisafiri kwa ndege kutoka nchi tano tofauti, mamlaka ya matibabu ya Uganda ilisema katika taarifa.
Watano walikuwa wametoka Nigeria, wawili kutoka Afrika Kusini - ambapo aina hiyo iliripotiwa mara ya kwanza - na wawili kutoka Falme za Kiarabu.
Siku ya Jumanne, matokeo ya utafiti uliochapishwa nchini Afrika Kusini yalionyesha shindano mbili za chanjo ya Pfizer ya Covid inatoa karibu asilimia 70 ya kinga dhidi ya kirusi cha Omicron.
Kuibuka kwa aina hiyo ya kirusi kulizua hofu kwamba inaweza kusababisha ugonjwa mbaya, maambukizo zaidi au kukwepa chanjo.
Viashirio vya awali vilionyesha kuwa inaweza kuambukizwa kwa haraka, lakini data ya kuzua matumaini kufikia sasa imependekeza kuwa chanjo bado hutoa kinga dhidi ya Omicron.