SERIKALI imeihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa itaendelea kuwekeza rasilimali fedha kwa ajili ya kutoa elimu kwa maendeleo ya nchi. Ahadi hiyo imetolewa mjini Dubai na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Lameck Nchemba kwenye kilele cha mkutano unaohusu uwekezaji kwenye sekta ya elimu katika karne ya 21.
Dk Nchemba amesema kuwa Serikali itaendelea kuongeza bajeti ya sekta ya elimu kila mwaka kadri rasilimali fedha inavyopatikana na kuiomba jumuiya ya kimataifa kuchangia juhudi hizo za Serikali.
Alisema kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mtoto anayetakiwa kwenda shule anapata elimu bila vikwazo kwa kutoa elimu bila malipo huku akiboresha mazingira ya shule nchini kote.
"Mhe. Rais Samia ameelekeza pia fedha zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF zitumike ipasavyo na zitaleta mapinduzi makubwa katika elimu nasi tumewahakikishia wadau wa maendeleo kwamba fedha watakazotupatia zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa" alisema Dk Nchemba
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alisema kuwa nchini Tanzania kuna utashi wa kisiasa wa kuendeleza elimu ambapo bajeti ya elimu imekuwa ikiongezeka kila mwaka na mpaka sasa imefikia zaidi ya asilimia 17 na kwamba huenda siku zijazo ikafikia asilimi 20 ya bajeti yote ya Serikali.
Mkutano wa masuala ya elimu ujulikanao kama WirED umewashirikisha wadau mbalimbali kutoka duniani kote ambapo hoja mbalimbali za kuboresha elimu, ikiwemo kuwawezesha vijana, na kuimarisha masuala ya teknolojia yamejadiliwa kwa kina katika mkutano huo.