Iran imemkamata mpwa wa kiongozi wa juu wa taifa hilo Ayatollah Ali Khamenei, miezi kadhaa baada ya kushiriki katika hafla na kumsifu mjane wa mfalme aliepinduliwa.
Farideh Moradkhan ni mtoto wa dada yake Khamenei, aitwaye Badri, ambaye alikosana na familia yake katika miaka ya 1980, na kukimbilia nchini Iraq wakati wa kilele cha vita kati ya Iran na Iraq.
Moradkhan, aliejizolea umaarufu kama mwanaharakati wa kupinga adhabu ya kifo, alikamatwa na vikosi vya usalama Alhamisi iliyopita, amesema kaka yake Mahmoud Moradkhan, alipozungumza Jumapili na Televisheni ya Kimataifa ya Iran, yenye makao yake mjini London.
Hakukuwa na taarifa za ndani juu ya sababu za kukamatwa kwake. Lakini baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamezungumzia tukio la Oktoba 2021, ambako Moradkhan alionekana akimsifu Farah Diba, mjane wa Shah Mohammad Reza Pahlavi, aliepinduliwa katika mapindizi ya Kiislamu ya mwaka 1979.
Moradkhan alitoa pia wito wa kurejea Iran kwa mjane huyo wa Shah, ili kuogoza kile alichokiita kuzaliwa upya kwa utamaduni wa Iran.
0 Comments