Kansela Scholz aiambia Urusi mipaka haihamishwi kwa nguvu

 


Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema mipaka ya Ulaya haistahili kuhamishwa kwa nguvu na kuongeza kuwa haiwezekani kukaa kimya tena baada ya miaka kadhaa iliyoshuhudia mivutano inayoongezeka katika mpaka wa Ukraine na Urusi. 

Katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya video katika Mkutano wa Kiuchumi Duniani, Scholz amesema ni mapema mno kusema iwapo Urusi itasaidia kupunguza mivutano iliyoianzisha na jirani yake mdogo. 

Kansela huyo wa Ujerumani lakini amedai kuwa Urusi inafahamu kwamba nchi za Magharibi ziko tayari kupunguza mivutano hiyo. 

Scholz ameyasema haya wakati ambapo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken, ametoa wito wa umoja kwa mataifa ya Magharibi kutokana na kile alichokiita uchokozi usiokwisha wa Urusi dhidi ya Ukraine. 

Katika ziara yake nchini Ukraine leo, Blinken amemuhakikishia Rais Volodymyr Zelenskiy kwamba Marekani na marafiki zake wataiunga mkono nchi hiyo.


Post a Comment

0 Comments