Vijana hao maarufu kama macharii wa R waliuawa Ijumaa Januari 7, 2022 katika eneo la Njiro jijini Arusha huku pikipiki yao ikichomwa moto.
Vijana hao, Anold Mushi (19) na Jumanne Selemani (17) wote wakazi wa eneo la California Sombetini jijini Arusha, wanadaiwa kuwa walikwapua pochi ya mwanamke ikiwa na vitu mbalimbali akiwa anapita njiani.
Inadaiwa kuwa baada ya kukwapua pochi hiyo wakiwa wanaendesha pikipiki iliyokuwa imepewa jina la tatu mzuka wananchi walianza kuwakimbiza hadi kuwakamata na baada ya kukamatwa vijana hao walipigwa hadi kufariki na pikipiki yao kuteketezwa na kuchomwa moto.
Vanessa Deo mama mzazi wa Anold na Khadija Selemani mama mzazi wa Jumanne walikiri kuuliwa kwa watoto wao na watu wasiojulikana.
"Mimi nilikuwa nyumbani nilipitiwa simu na kaka yake Anold ambaye aliniambia mtoto wangu amepata shida na baadaye nikiwa najindaa kwenda polisi nilijulishwa tayari ameuawa"amesema
Amesema Anold licha ya kuendesha bodaboda alikuwa akifanyakazi kazi za ufundi wa nyumba na kutengeneza thamani za ndani.
Khadija amesema mtoto wake alikuwa anafanya kazi ya bodaboda na alipata taarifa za kuuawa baada ya kutoonekana nyumbani.
Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha Justine Masejo amethibitisha kuuawa kwa waendesha bodaboda hao lakini ameonya wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi.
0 Comments