SERIKALI ya Norway kupitia Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD), imetoa msaada wa Dola za Marekani milioni tatu kwa Tanzania kwa ajili ya kufadhili mradi wa kujengea uwezo kwa taasisi zinazohusika na masuala ya mazingira ili kupunguza hewa ukaa inayosababishwa na ukataji miti na uharibifu wa misitu.
Mratibu Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Hifadhi ya Mazingira (IUCN), Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Charles Uluchina alisema hayo jana mjini Morogoro wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo wa awamu ya pili.
Uluchina alisema Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini inasimamia nchi 24 ambayo ni wanachama wa Shirika hilo na mradi huo wa miaka mitatu endapo utafanikiwa, Serikali ya Norway itaweza kuongeza miaka mingine mitano ya utekelezaji wake.
Mratibu Mkazi wa Shirika hilo, alisema mradi huo unaojulikana kwa jina la REDD+READY unaangalia jinsi ya matumizi ya mazingira na ardhi ya wakulima inavyoweza kuwa endelevu ili makali yanayotokana na uharibifu wa mazingira yaweze kupungua.
Uluchina alisema mradi huo utatekelezwa na Mpango wa Kukuza Kilimo Ukanda Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), katika maeneo ya Ifakara wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro na Ihemi iliyopo mkoani Iringa.
Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Andrew Komba alisema mradi huo wa awamu ya pili ni kwa ajili ya kujenga uwezo wa kitaasisi ambazo zina wajibu wa kutekeleza mradi huo kuanzia kwenye jamii, wizara mtambuka zikiwemo Tamisemi, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Maliasili na Utalii ambapo kwa pamoja watautekeleza.
Dk Komba alisema chini ya mradi huo mambo yatakayoangaliwa ni pamoja na Sheria, Kanuni na Sera ili kila taasisi na mdau awe na uwezo wa kutekeleza afua zinazohusiana na masuala ya uhuishaji wa misitu.
Kwa upande wa uharibifu wa mazingira na misitu, Dk Komba alisema hali ilivyo kwa sasa wastani wa hekta 469,000 zinakatwa kwenye misitu nchini kwa ajili ya matumizi mbalimbali yanayohusiana na utafutaji wa nishati kwa ajili ya kupikia, kujengea na matumizi mengine.
“Kasi hii ya ukataji miti sio nzuri kwa maendeleo ya mustakabali wa mazingira yetu na kwamba mradi huu unakuja kuchangia kuwa na malengo ya kupunguza uharibifu wa mazingira na kutafuta nishati mbadala na kufanya kilimo ambacho kinazingatia uhifadhi wa mazingira,” alisema Dk Komba.
Akizindua mradi wa REDD+READY, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga alisema kupitia mradi huo, ofisi ya Makamu wa Rais itahakikisha misitu haiharibiwi na kuweka mkakati endelevu wa kupanda miti, kuitunza na kutunza vyanzo vya maji.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais alisema Mabadiliko ya Tabianchi yapo na kuendelea kukabiliana nayo, kwa vile ardhi bado ipo juhudi mbalimbali zitachukuliwa kwa ajili ya kurejesha uoto wa asili ili vizazi vijavyo viweze kunufaika.
0 Comments