F Nauli za mabasi ya mikoani daladala zikipanda | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Nauli za mabasi ya mikoani daladala zikipanda

 


Ni maumivu kotekote, baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) kutangaza viwango vipya vya nauli kwa mabasi ya mikoani na daladala.


Kutokana na kilio cha muda mrefu kutoka kwa wamiliki wa mabasi, daladala hata malori kuhusu gharama za uendeshaji, Latra ilikifanyia kazi jana kwa kuwataka Watanzania kulipa zaidi, ingawa wanafunzi wataendelea kutozwa Sh200 iliyokuwapo.


Akitangaza viwango hivyo vipya, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliard Ngewe alisema vitaanza kutumika baada ya siku 14 na watoa huduma za usafiri watapaswa kuwafahamisha abiria kupitia vyombo vya habari.


Kwa daladala, alisema umbali wa mpaka kilomita 10 nauli itakuwa Sh500 badala ya Sh400 iliyopo na waliokuwa wanalipa nauli ya Sh450 itakuwa ni Sh550.


“Kwa kilomita 30 nauli itakuwa Sh850 badala ya Sh750 inayotozwa sasa, kwa kilomita 35 nauli itakuwa Sh1,000 na kwa kilomita 40 nauli itakuwa Sh1,100,” alisema Ngewe.


Kwa mabasi ya mkoani daraja la kawaida kila abiria atalipa Sh41.29 kutoka Sh39.89 iliyopo kwa umbali wa kilomita moja sawa na ongezeko la Sh4.4 au asilimia 11.92.


“Kwa daraja la kati, abiria atatozwa Sh56.88 kwa kila kilomita moja badala ya Sh53.22. Kiwango kilichoongezwa ni Sh3.66 sawa na asilimia 6.88,” alisema Ngewe.


Viwango vya nauli kwenye barabara za vumbi alisema zitapanda kwa asilimia 25 ya daraja la kawaida kwa barabara za lami ambayo ni sawa na Sh51.61 kwa abiria mmoja kwa kila kilomita.


“Kwa mujibu wa kanuni ya 19 ya ya Latra ya mwaka 2020, watoa huduma wanatakiwa kutoa matangazo ya nauli mpya kwa siku 14 kabla ya kuanza kutumia nauli mpya. Taarifa hiyo itolewe kwenye vyombo vya habari,” alisema Ngewe.


Hata hivyo, wadau wa usafiri wamepongeza uongezaji wa viwango vya nauli, ingawa bado ni vidogo kulinganisha na gharama za uendeshaji, ikiwamo bei ya vipuri.


Mweka hazina wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Issa Nkya alisema wameupokea vizuri uamuzi huo, ingawa hayakuwa matakwa yao kutaka nauli zipande ila wanafanya hivyo kulingana na gharama halisi za uendeshaji.


“Lengo letu sio kukomoana kwa kutoa huduma kwa abiria, japo tumepunjwa hatutaki kuumiza wananchi, hakuna asiyefahamu kuwa vifaa vimepanda bei,” alisema Nkya.


“Kiwango kilichoongezwa ni kidogo, lakini hatuachi kutoa huduma. Bado kuna sheria kandamizi Latra, ikiwamo tozo anayotozwa mmiliki. Tutaendelea kuomba sheria hizi ziondolewe,” alisisitiza.


Mweka Hazina wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Julius Munis alisema kiasi cha nauli kilichoongezwa ni kidogo ukilinganisha na gharama za uendeshaji.


Alisema waliomba ongezeko la nauli, angalau litoke Sh400 hadi Sh600 kutokana bei ya vipuri kuongezeka na kupanda kwa ma-futa.


Kaimu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Usafiri Ardhini (Latra CCC), Leo Ngowi alisema wamepokea uamuzi huo kwani viwango vilivyowekwa vinaendana na hali halisi ya maisha ya Mtanzania.


Walichokisema wachumi

Kupanda kwa nauli za mabasi, wadau wanasema kutapandisha bei ya kila kitu, zikiwamo bidhaa muhimu, hivyo kuongeza ukali wa maisha.


Baada ya Latra kutangaza nauli mpya za mabasi na daladala jana, mabadiliko hayo yatagusa usafirishaji wa mizigo pia.


Baadhi ya wasafirishaji na wachumi, wamesema gharama za maisha zinakwenda kupanda kutokana na ongezeko la bei ya mafuta kulikochangia kupandisha nauli, wakisema badiliko lolote la gharama za uzalishaji na uendeshaji, linazigusa bidhaa pia.


Mathalan, wamesema gharama za kusafirisha ndizi kutoka Rombo mkoani Kilimanjaro kwenda Dar es Salaam zitapanda kama ilivyo kwa mchele unaolimwa Ubaruku mkoani Mbeya kwenda mikoa mingine, hata bidhaa za viwandani zinazonunuliwa zaidi kutoka Soko la Kimataifa Kariakoo kwenda mikoani.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Repoa, Dk Donald Mmari alipendekeza hatua tatu zinazoweza kuchukuliwa na Serikali kupunguza makali ya bei, ikiwamo kushusha baadhi ya kodi kwenye bajeti mpya.


“Chimbuko ni vita vinavyoendelea kati ya Urusi (Russia) na Ukraine. Kwa sababu supply (usambazaji) ya mafuta duniani imepungua. Kumbuka Urusi ni mzalishaji mkubwa wa mafuta duniani,” alisema Dk Mmari na kuongeza:


“Sasa yuko (Urusi) kwenye vita na amewekewa vikwazo, hivyo mafuta yanayoingia sokoni ni machache kuliko mahitaji kwa hiyo bei inapanda katika soko la dunia. Hakuna nchi yenye control (udhibiti),” alisema.


Athari za vita hivyo sio tu imeigusa Tanzania, mchumi huyo mwandamizi alisema hata Marekani, sasa hivi wananchi wananunua galoni moja kwa dola tano (takriban Sh12,000), bei kubwa ambayo haijawahi kutokea miaka ya hivi karibuni.


“Serikali inachoweza kufanya ni kuangalia aina ya kodi ambazo zinaweza kupunguzwa. Kwa kuwa Serikali ndio inasoma bajeti mpya ya mwaka 2022/23. Lakini hakuna control na bei ya mafuta,” alisema.


Kingine, Dk Mmari alisema ni kuwa na akiba ya kutosha ya mafuta ili kunapokuwa na mshtuko kama uliojitokeza itumike kupunguza makali.


“Eneo la tatu ni kuangalia kutoa nafuu kwa wawekezaji wanaozalisha baadhi ya bidhaa ili zizalishwe kwa wingi nchini hivyo kupunguza utegemezi kutoka nje,” alisema.


Dk Mmari alifafanua kwamba bidhaa zinazotoka nje mfano ngano na mafuta ya kula yanapanda bei kwa sababu huduma za uchukuzi nazo hupanda, hata kipindi hiki cha vita vya Russia.


“Container (kasha) walilokuwa wakilisafirisha kwa dola 2,000 za Marekani sasa hivi ni kati ya dola 5,000 hadi dola 8,000,” alisema.


Conrad Kabewa, mchambuzi wa masuala ya biashara na uchumi alisema mafuta huingia katika gharama za uendeshaji na uzalishaji, hivyo mzalishaji hawezi kuuza bidhaa kwa bei ileile, kwani atapata hasara.


“Lengo la mfanyabiashara yeyote ni kupata faida, kwa hiyo hawezi kubaki na bei ya zamani wakati gharama za kusafirisha bidhaa zimepanda kutokana na bei ya mafuta. Hii kitu inakwenda kupandisha bei ya kila kitu,” alisema.


Aliongeza kwamba gharama za usafiri zikipanda hugusa kila eneo kwa hiyo bei za bidhaa zitapanda. Kama gharama za kusafirisha vitunguu imepanda kutoka mfano Sh500,000 hadi Sh700,000 lazima bei itapanda sokoni.


“Sasa hivi umeme wetu sio wa uhakika, unakatikakatika sana kwa hiyo kuna baadhi ya wazalishaji wanalazimika kuwasha majenereta na yanatumia mafuta ambayo bei yake iko juu kwa sasa, unategemea atauza kwa bei ya zamani?” alihoji.


Kwa mujibu wa Kabewa, wazalishaji na wasafirishaji wa bidhaa hawatakuwa tayari kubaki na bei za zamani wakati gharama za uendeshaji zimepandishwa na mafuta, atalipia mlaji wa mwisho.


Kuhusu mwenendo wa bei ya bidhaa na huduma nchini, Mkurugenzi wa Shahada za Juu wa Chuo cha Usimamizi wa Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory alisema hali iliyopo sasa itaendelea, hivyo mpaka bei ya mafuta itakapotulia kwani ndio chanzo cha mabadiliko yanayoshuhudiwa.


“Kuongezeka kwa bei za vitu na huduma kutaendelea kwa sababu mafuta yanaendelea kupanda, bei ya bidhaa inatokana na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na uzalishaji ambayo inahusisha mafuta pia,” alisema Dk Pastory.


Alisema namna ya kunusuru hali hiyo ni Serikali kuweka ruzuku au kuangalia namna ya kupunguza kodi zilizopo ili kupunguza bei yake kwa kuwa athari ya mafuta inagusa sekta zote.


Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Delphin Rwegasira alisema gharama za bidhaa zinapanda kutokana na jiografia ya nchi na muundo wa uchumi ambao unategemea viwanda na uzalishaji mashambani.


“Uchumi wetu unategemea viwanda na kilimo, hivyo lazima bidhaa zisafirishwe kwenda mashambani. Nchi yetu ni kubwa na pana sana, kutoa bidhaa sehemu moja kwenda nyingine ni gharama hususan wakati huu ambao gharama za mafuta ziko juu,” alisema Profesa Rwegasira.


Mchumi huyo aliongeza kuwa kuna uwezekano usio wa moja kwa moja kuwa kuongezea kwa bei ya bidhaa na huduma kukaathiri uzalishaji viwandani na mashambani, kwani malighafi na pembejeo muhimu lazima zisafirishwe.


Wananchi wafunguka


Mmiliki wa nyumba ya kulala wageni jijini hapa, Said Watua alisema anakusudia kuongeza bei ya malazi katika nyumba yake kwa sababu ya kupanda kwa gharama za bidhaa mbalimbali, zikiwamo sabuni za kufulia na dawa za chooni, jambo ambalo linaongeza gharama za uendeshaji.


“Hata sisi tunaathirika na kupanda kwa bei, kwenye guest yetu tuna mashuka ambayo yanahitaji kufuliwa, ukiuliza sabuni za kufulia sasa zimepanda bei. Bafuni tunaweka sabuni za kuogea, nazo pia zimepanda lakini bei zetu bado ni zilezile. Tunaangalia hali inavyokwenda, ninafikiria kupandisha bei ili nami nipate faida. Gharama ni kubwa kama ilivyo kwa watu wengine huko mtaani,” alisema mfanyabiashara wa Kinondoni.


Aloyce Makalanga, mkazi aliyepanga nyumba Tabata alisema hashangai kuona nauli za daladala zimepanda kwa sababu kila kitu kimepanda bei mitaani.


“Kitu pekee ambacho hakijapanda bei ni kodi ya nyumba pale ninapoishi. Sijui siku moja mwenye nyumba akiniambia anapandisha kodi itakuwaje, hali ni tete. Serikali itusaidie tupate unafuu wa maisha,” alisema Makalanga.


Kwa upande wake, mfanyabiashara katika Soko la Ilala, Gilbert Thadeo alisema ongezeko la nauli litamwongezea maumivu kwa sababu amekuwa akipeleka bidhaa kwa wateja wake katika maeneo mbalimbali.


“Hii biashara yetu ya mitumba wakati mwingine tunatakiwa kupeleka mzigo kwa mteja wa Mbagala, Gongo la Mboto au Kigamboni. Sasa kama nauli imeongezeka hivyo, hata gharama za usafirishaji wa mizigo pia zitaongezeka, hali itakuwa ngumu kwa kweli,” alisema.


Wadau wengine

Akizungumzia nauli mpya zilizotangazwa, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (Tapia), Mahmoud Mringo alisema hata wazazi wanapaswa kuongeza nauli kwenye mabasi ya shule.


“Kwa sasa ndiyo tumemaliza Sikukuu ya Pasaka, shule nyingi zilifungwa na zimefunguliwa hivi karibuni. Wamiliki wa shule tutakaa kisha tutafanya vikao na wazazi na kuona tunakwendaje,” alisema.


Mringo alisema kuongezeka kwa nauli hizo kutategemea na shule husika, kulingana na mmiliki anavyoendesha biashara yake.


“Hii ni athari ya vita ya Urusi na Ukraine, ni vita vya uchumi wao. Wanarushiana silaha sisi tunalipa gharama, kuna hatari hata ya huduma kufungwa iwapo hali itaendelea kuwa hivi,” alisema Mringo.


Katika shule nyingi, kwa sasa wazazi hulipa Sh120,000 kwa muhula wa miezi kwa ajili ya usafiri wa mwanafunzi anayeishi ndani ya kilomita tano kwa shule nyingi za Dar es Salaam.


Ramadhan Mbena, dereva wa mtu binafsi alisema kuongezeka kwa gharama za nauli ni nafuu kwa wafanyabiashara wa sekta hiyo, lakini wao wanaendelea kuugulia.


Alisema mabosi wao huwapa fedha kwa ajili ya mafuta yatakayotosha safari yenye umbali fulani na tangu bei ya bidhaa hiyo iongezeke hawakuwahi kuongezewa.


“Kwa mfano wakati ule tukiwa tunakwenda Dodoma bosi anataka umfuatie mzigo wake au umpelekee barua atakupa Sh200,000 ya mafuta, lakini sasa tunapewa kiasi hicho unanunua mafuta hupati hata hela ya kuacha nyumbani, wao hawatuelewi,” alisema.


Alisema dereva yeyote atakayemlalamikia bosi wake ananyang’anywa funguo na kuachishwa kazi.


“Hatuna pa kulilia, hatujui tufanyeje maana tunaendesha magari ya watu binafsi na ni gari binafsi sio la mizigo, hatima ya ajira yako ipo mikononi mwa bosi wako, mafuta yamepanda tunaumia,” alisema.


Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki Wadogo wa Malori Tanzania (Tamstoa), Chuki Shaaban alisema kuongezeka kwa nauli kunaendana na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji wa mizigo kutoka ndani ya nchi kwenda nje.


“Baada ya bei ya mafuta kupanda wamiliki wa malori ilitupasa kutoza mizigo kulingana na gharama za uendeshaji, hawa wenzetu wamefikia uamuzi huo kulinda maslahi yao, ni jambo jema lakini maumivu anayapata mwananchi,” alisema.


Hata hivyo, Shaaban alitilia shaka kupanda ghafla kwa bei ya mafuta, alisema inashangaza vita ilivyoanza na mafuta yalipanda papo hapo.


“Kwa sasa ni sawa, lakini vita vya Urusi na Ukraine ni kichaka ambacho watu walijifichia ila ukweli kuna mambo ya kibiashara, haiwezekani vita ianze leo na mafuta yapande leo, ina maana hatukuwa na akiba?” alihoji.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Hassan Mchanjama alisema ongezeko hilo ni ushindi kwa chama hicho, kwani ni nafuu ukilinganisha na ilivyopendekezwa na watoa huduma.


Alisema baada ya taarifa hiyo, Chakua wanajiandaa kufanya mkutano wa kukusanya maoni ya wadau kujua iwapo wameridhika ama la.


“Ongezeko hili ni ushindi kwa Chakua, watoa huduma waliomba iongezwe mara mbili ya ilivyo sasa, hii ingewaumiza abiria, lakini kilichoongezwa ni kidogo hasa kwa usafiri wa daladala, tunashukuru.


“Ukiangalia kilichoongezwa hapo ni Sh50 katika safari za chini ya kilomita 10, kwa maana iliyokuwa inalipwa Sh400 sasa italipwa 500 na ile ya 500 sasa italipwa 550, nauli za wanafunzi zimebaki kuwa Sh200, hii tofauti na watoa huduma walivyotaka, walitaka safari ya 400 ilipwe 800, kwa hiyo huu ni ushindi kwa abiria,” alisema.


Post a Comment

0 Comments