TBS yasisitiza wazalishaji wa bidhaa kuzingatia viwango na ubora kufikia soko la nje

 


Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewakumbusha wajasiriamali wakubwa na wadogo kuhakiki ubora wa bidhaa zao pamoja na  kuhakikisha wanaweka vifungashio vyenye ubora ili kuvutia sokoni.


Pia imewakumbuisha kutengeneza bidhaa ambazo zinakidhi soko la kitaifa na kimataifa.

Hayo yameelezwa leo Agosti 6 mwaka huu na Meneja wa kanda ya kati wa shirika hilo,Nickonia Mwabuka wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la shirika hilo lililopo  nane nane Nzuguni Jijini Dodoma.

TBS ipo katika maonesho hayo na imekuwa ikitoa elimu kwa watanzania kuhusu kazi zinazofanywa na shirika hilo ikiwemo ile ya kuhakikisha kuwa bidhaa zote zinazoingia Tanzania zinakidhi usalama wa afya.

Mwabuka amesema  wajasiriamali wakubwa na wadogo wana wajibu wa kuhakikisha wanaweka vifungashio vyenye ubora ili kuvutia sokoni na ndani na nje ya Tanzania.

“Kama tutakuwa na bidhaa ambazo ni hafifu soko letu la Tanzania litavamiwa tunawasihi na kuwakumbusha wajasariamali waje wahakiki ubora wa bidhaa zao.

Amesema katika banda lao wanatoa elimu kwa wajasiriamali lengo likiwa ni kuhakikisha wanatoa bidhaa zenye ubora na zenye mahitaji ya soko husika.

“Kilimo ni biashara, kwenye biashara ni lazima uwe na biashara zinazokidhi viwango vya ndani na nje ya nchi.Kumbuka kwamba Tanzania ni wanachama  wa Jumuiya ya  Afrika Mashariki na pia ipo SADC   mahitaji ni makubwa bidhaa lazima zikidhi vigezo,”amesema Meneja huyo wa Kanda.


Katika hatua nyingine,Meneja huyo amesema TBS imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 250 kwa ajili ya kutoa elimu kwa wajasirimali kuhusu umuhimu wa kutengeneza bidhaa zenye ubora.

“Lakini pia wajasiriamali wakubwa nao pia tunawapa  elimu ya ubora lakini kubwa ambalo tunazingatia ni suala la vifungashio katika bidhaa zetu.

“Na Waziri wa Mifugo na Uvuvi alizungumzia kwa undani lazima vifungashio  vikidhi vigezo na soko letu litakuwa halina ushindani,”amesema meneja huyo.

Hata hivyo amewataka waandishi wa habari kuendelea kuwakumbusha watanzania kutengeneza bidhaa zenye kukidhi matakwa ya viwango ili waweze kushindana ndani na nje ya nchi.

Post a Comment

0 Comments