Wakaazi wa maeneo ya magharibi mwa Ethiopia wanasema watoto wamekuwa wakifa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa surua kwa muda wa miezi michache iliyopita kutokana na changamoto ya kufikia huduma za afya.
Waliozungumza na BBC wanasema vizuizi vya barabarani vilivyowekwa kutokana na mzozo unaoendelea katika eneo hilo vimetatiza harakati.
Serikali ya muungano imekuwa ikipambana na uasi mbaya magharibi mwa Oromia - ngome ya waasi wa Oromo Liberation Army (OLA).
Afisa wa afya Dereje Abdena alithibitisha kwa BBC kuhusu milipuko ya wa magonjwa ya surua na malaria katika eneo hilo - ikiwa ni pamoja na katika maeneo yaliyokumbwa na ukame.
Mamlaka zinasema ziko katika harakati za wakijaribu kuwafikia walioathirika.
"Siku chache tu zilizopita tulizika watoto wawili waliofariki kutokana na surua. Madaktari wameondoka eneo hilo," mkazi wa wilaya ya Kondala katika eneo la Wollega Magharibi alisema.
Surua inasambaa kwa kasi sana na inaweza kusababisha ugonjwa mbaya.
Katika ripoti ya hivi majuzi, Umoja wa Mataifa ulisema hali ya kibinadamu katika eneo la Oromia magharibi "bado ni ngumu" huku maelfu wakikosa makazi kutokana na migogoro.
‘’Upatikanaji, usalama na rasilimali bado ni changamoto kufikia idadi ya watu walioathirika,” Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilisema.
0 Comments