Ticker

6/recent/ticker-posts

Vita vya Ukraine: Zelensky alaani 'ugaidi' wa Urusi katika hotuba ya Umoja wa Mataifa


Rais Volodymyr Zelensky ameishutumu Urusi kwa "uhalifu dhidi ya binadamu" baada ya mashambulizi mapya ya makombora kusababisha kukatika kwa umeme kote Ukraine.


Aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia kiunganishi cha video kwamba "mfumo wa ugaidi" wa Urusi ulilazimisha "mamilioni ya watu kukaa bila vifaa vya nishati, bila joto, bila maji" kwenye baridi ya chini ya sufuri.


Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya takriban watu saba, Ukraine ilisema.


Mitambo ya nyuklia ilizimwa.


Mitambo hiyo mitatu ambayo bado iko chini ya udhibiti wa Ukraine ilikatwa kutoka kwa gridi ya taifa na mtambo wa Zaporizhzhia - mkubwa zaidi barani Ulaya - ulilazimika tena kutegemea jenereta za dizeli kuwezesha mifumo yake ya kupoeza na vifaa muhimu vya usalama.


Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limeelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu mtambo wa Zaporizhzhia unaodhibitiwa na Urusi, ambao umepata madhara kutokana na kushambuliwa kwa makombora mara kwa mara.


Nchi jirani ya Moldova pia ilikumbwa na kukatika kwa umeme siku ya Jumatano, lakini haikupigwa moja kwa moja.


Wakati majira ya baridi yakianza, Moscow imeongeza mashambulizi kwenye miundombinu ya nishati ya Ukraine.

Post a Comment

0 Comments