Israel kuruhusu 'kila raia' kutembea na bunduki kujilinda

 


Baraza la usalama la Israel limeidhinisha hatua za kuwarahisisha Waisraeli kubeba bunduki baada ya mashambulizi mawili tofauti ya Wapalestina mjini Jerusalem katika muda wa siku mbili zilizopita.


Mashambulizi hayo yametokea baada ya jeshi la Israel kuvamia Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kuua watu tisa.


Hatua hizo mpya pia ni pamoja na kuwanyima wanafamilia wa mtu atakayebainika kushambulia haki ya ukaaji na hifadhi ya kijamii.


Baraza la mawaziri linatarajiwa kuthibitisha hatua hizo leo Jumapili. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alikuwa ameahidi kujibu mapigo tena ya "haraka" kabla ya mkutano wa baraza la mawaziri la usalama.


Jeshi la Israel pia lilisema litaongeza idadi ya wanajeshi katika Ukingo wa Magharibi. "Wakati raia wakiwa na bunduki, wanaweza kujilinda," Waziri wa Usalama wa Kitaifa mwenye utata wa mrengo mkali wa kulia Itamar Ben-Gvir, aliwaambia waandishi wa habari nje ya hospitali ya Jerusalem.


Hatua hizo zitafutilia mbali haki za usalama wa kijamii za "familia za magaidi wanaounga mkono ugaidi", baraza la mawaziri la usalama lilisema.


Mapendekezo hayo yanaenda sambamba na mapendekezo ya washirika wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Bw Netanyahu, waliomruhusu kurejea mamlakani mwezi uliopita.


Tangazo hilo limekuja baada ya polisi wa Israel kusema mvulana wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 13 ndiye aliyehusika na ufyatuaji risasi katika kitongoji cha Silwan mjini Jerusalem siku ya Jumamosi na kusababisha baba na mwana wa Israel kujeruhiwa vibaya.


Msemaji wa jeshi la polisi la Israel hapo awali alisema mshambuliaji aliwavizia watu watano walipokuwa wakielekea kwenye maombi, na kuwaacha wawili katika "hali mbaya".


Mshambuliaji huyo aliuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la tukio. Mwanamume aliyehusika na shambulio la siku ya Ijumaa katika nyumba ya ibada alitambuliwa na vyombo vya habari kuwa ni Mpalestina kutoka Jerusalem Mashariki. Polisi wamewakamata watu 42 kuhusiana na shambulio hilo.

Post a Comment

0 Comments