KIKWETE ATAKA WANANCHI KUSHIRIKISHWA UTWAAJI ARDHI.

 


Na Deborah  Lemmubi - Dodoma


Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewataka Wataalam wa Mipango miji kutambua kuwa zoezi la utwaaji Ardhi ni la ushirikishwaji tofauti na baadhi ya wataalam wanavyofanya bila kushirikisha Wananchi.


Na kuongeza kuwa vitendo hivi havikubaliki na kuitaka bodi ya wataalam wa mipango miji kutoa elimu kwa wataalam hao kuacha tabia hiyo inayochangia kuleta migogoro mikubwa kwa wananchi hususani katika maeneo ya miji ambapo miradi ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi imekuwa ikiendelea.


Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Waziri Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Ridhiwani Kikwete wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya usajili wa wataalam wa Mipango miji Sambamba na ukabidhi wa vitendea kazi kwa Wajumbe wapya wa Bodi,na kusema kuwa ni vibaya sana kwa wataalam hao kukiuka taratibu za kitaaluma suala linalopekea wanasiasa kuingilia kati ili kutoa maamuzi ambayo yanaweza kuchochea migogoro kwani wanasiasa sio wataalam wa fani hiyo.


Ridhiwani Kikwete pia ameonya tabia ya kutosimamia mipango miji waliyoiweka inasababisha miji kuvurugwa kwani kwasasa kila mahali kuna ujenzi wa vyumba vya maduka au vituo vya mafuta na baa katika makazi ya watu.


‘’Haya ni mambo ambayo Bodi inapaswa kuyasimamia kwani uzinduzi wa Bodi hii ni suala muhimu sana katika mustakabali wa ukuaji wa taaluma ya Mipangomiji, kwani Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya Bodi ndizo pande mbili ambazo zinaungana pamoja katika kuikuza na kuisimamia taaluma ya mipangomiji nchini’’.


Aidha Kikwete ameitaka bodi hiyo kuzingatia uzoefu na weledi wajumbe wa Bodi hiyo walionao katika fani mbalimbali, kushirikiana kikamilifu na Wizara kuendeleza taaluma ya Mipangomiji kwa pamoja na kufikia lengo la kusimamia Wataalam wa Mipangomiji na kampuni za upangaji miji.


‘’Usimamizi wenu utafanya Wataalam na Kampuni za Mipangomiji zifanye kazi kwa weledi na kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za upangaji miji, kutoa huduma bora, kuweka mazingira ya kuvutia Wataalam wa Mipangomji waliokidhi vigezo vya kusajiliwa ili wasajiliwe, pia kuzalisha fursa zaidi za ajira na kuongeza mchango katika pato la Taifa.’’


Naibu Waziri Kikwete amesema Sekta ya Ardhi ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa na kwa kila mwananchi akiongeza kuwa Ardhi ni msingi wa kipekee wa maendeleo na ni rasilimali isiyoongezeka.


Akitolea mfano wa Nchi yetu Naibu Waziri Kikwete amesema Tanzania ina eneo lenye ukubwa wa takribani kilometa za mraba 948,132.89, ikijumuisha kilometa za mraba 62,032.89 za maji uku eneo la nchi kavu lina ukubwa wa kilometa za mraba 886,100, ambapo Tanzania bara ni kilometa za mraba 883,600, na Zanzibar ni kilometa za mraba 2,500.


Na kuongeza kuwa kuna ongezeko la watu kutoka watu 43,625,354 Sensa ya watu 2012, hadi kufikia watu 61,741,120 Sensa ya Watu na Makazi 2022 wakati idadi ya watu ikiongezeka, ukubwa wa ardhi bado ni ule ule.


Kwa upande wa mijini Naibu Waziri huyo amesema, matokeo yake yamejidhihirisha kupitia ongezeko la uendelezaji wa miji isiyopangwa na ukuaji wa makazi holela na kuitaka bodi kufanyia kazi changamoto hizi ili zitatuliwe kwa kupanga ardhi mijini na vijijini ili uendelezaji miji ufuate mipango ya matumizi ya ardhi.


Aidha, Naibu Waziri Kikwete ameitaka bodi pamoja na wataalam wa Mipango Miji kubuni mbinu za namna bora ya kuimarisha utendaji kazi wa Wataalam na Kampuni za Upangaji Miji pamoja na kuibua mikakati ya kutatua changamoto zinazoikabili taaluma ya mipangomiji na Sekta ya Ardhi kwa ujumla, hasa utatuzi wa migogoro ya ardhi.


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Sheushi Mbuli aliyemwakilisha Katibu Mkuu Wizara hii Dr Allan Kijazi ameitaka Bodi hii mpya kusimamia kwa weledi eneo la maadili kwa kuangalia kwanini wataalamu wanakiuka Maadili ili wajue tatizo na kulishughulikia.


Naye Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo Prof. John Lupala akitoa mwelekeo wa bodi yake amesema Bodi kwa mwaka wa fedha ujao itaanzisha mfumo wa kufuatilia wataalamu wa mipangi miji ili kuweza kuwafuatilia kwa akaribu ili kuwazawadia wanaofanya vizuri na kutoa adhabu kwa wale wanaokiuka taratibu na maadili pia.


Prof. Lupala ameongeza kuwa Mfumo huu pia utawezesha bodi kuona kwa karibu kinachoondelea kwa wataalamu wa mipango miji lakini pia kuhakikisha wanaanza taratibu za usajili kwa wataalamu wa wapya kuanzia taratibu za awali mpaka usahili kwa wataalami hao.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete akikabidhi vitendea kazi kwa mjumbe mpya wa Bodi ya usajili Wataalam wa Mipango Miji Bw. Goodluck Mighonu mara baada ya kuzindua bodi hiyo leo Jijini Dodoma.


Bodi hii ni ya tatu na iliteuliwa Disemba 2022 chini ya Mwenyekiti wake  TP. Prof. John Lupala.

Post a Comment

0 Comments