Marekani yafuta Kitengo maalumu cha Polisi ‘Scorpion’ kutokana na mauaji ya raia

 


Idara ya Polisi ya Memphis imekivunja kitengo maalum cha Polisi kinachoitwa Scorpion, ambacho maafisa wake wanatuhumiwa kumuua Tire Nichols.


Scorpion ni jina linalomaanisha "Operesheni ya Uhalifu wa Mitaani ili kurejesha amani kwenye makazi ya watu".


Kitengo hiki cha watu 50 kilizinduliwa Oktoba 2021 kwa lengo la kupunguza viwango vya uhalifu katika maeneo fulani korofi, ikiwepo uporaji, wizi wa magari na kwenye maduka makubwa.


Lakini sasa kinafutwa baada ya maafisa wake kuonekana wakimpiga Bw Nichols, 29, kwenye video zilizosambaa kuanzia tarehe 7 Januari.


Katika taarifa yake, idara hiyo ilisema "ni kwa manufaa ya wote ni kukifuta kabisa" kitengo hicho.


"Ingawa vitendo viovu vya wachache vinaleta wingu la aibu kwa jina Scorpion, ni muhimu kwamba sisi, Idara ya Polisi ya Memphis, tuchukue hatua za haraka katika mchakato wa uponyaji kwa wote walioathiriwa," iliongeza.


Familia ya Bw Nichols ilikaribisha uamuzi huo katika taarifa kutoka kwa mawakili wao, na kuuita "unafaa na na haki kwa kifo cha kusikitisha cha Tire Nichols, na pia uamuzi wa heshima na wa haki kwa raia wote wa Memphis".


Maafisa hao watano - Tadarrius Bean, Demetrius Haley, Desmond Mills Jr, Emmitt Martin III na Justin Smith - walifutwa kazi wiki iliyopita.


Waliwekwa rumande siku ya Alhamisi na kila mmoja anakabiliwa na mashtaka ya mauaji, unyanyasaji mbaya, utekaji nyara uliokithiri, utovu wa nidhamu na ukandamizaji.


Mawakili wa Bw Martin na Bw Mills wamesema wateja wao watakana mashtaka.

Post a Comment

0 Comments