Marsabit wataka chakula cha misaada kisitishwe


Tangu ripoti za kupotea kwa zaidi ya magunia 100 ya chakula cha msaada kilichotarajiwa kuwafikia wananchi kutoka ghala la serikali eneo la Sololo jimboni Marsabit kuanza kuenea, wadau wanaonekana kukerwa na hali hiyo wanayosema "ni njama ya watu wachache kujinufaisha na chakula kinachonuiwa kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na hali mbaya ya ukame na ukosefu wa chakula."


Wananchi wamekuwa wakiomba msaada wa chakula kila uchao na ripoti za kupotea kwa chakula kilichonuiwa kuwasaidia,z imezua hamaki miongoni mwa wakaazi wa Marsabit.


Soma zaidi: Mifugo waangamia Kenya kwa kula mifuko ya plastiki


Kulingana na Seneta Marsabit Mohammed Chute, wakati umewadia kwa serikali kusitisha usambazaji wa chakula na badala yake "kuanza kuwapa wahanga wa baa la njaa pesa ili wajinunulie vyakula wenyewe."


“Mambo ya chakula ni shida. Chakula kinaibiwa barabarani, kinaibiwa hata kwenye maghala na, kwa hivyo, njia rahisi ya kufikisha chakula kwa watu ni kupitia mpango wa usambazaji wa pesa…" Alisema seneta huyo wa Marsabit wakati akizungumza na DW.


Wakaazi kutoka Sololo na maeneo mengine ya Marsabit wamekuwa wakiiomba serikali kuwapa msaada wa maji na chakula kutokana na makali ya ukame ambao umeendelea kuangamiza mifugo.


Katika eneo la bunge la Moyale, wakaazi wameikosoa serikali kwa kushindwa kuwapa msaada wakati huu wa ukame.


"Shida yetu ni maji na chakula.Serikali haitusaidii na tunahangaika kila wakati kutokana na uhaba wa maji na chakula." Alisema mmoja wa wakaazi wa hapo, Abdikadir Dido.


Naibu Kamishna wa eneo la Sololo, Robert Nzuki, amethibitisha kupotea kwa chakula kutoka kwenye ghala la serikali na kuonya kwamba "hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya waliohusika."


"Ni kweli kuna chakula kilipotea na wale ambao walihusika watafikishwa mahakamani. Inasikitisha kwamba chakula kinapotea wakati huu ambapo makali ya kiangazi yamezidi."


Wizi wa chakula kutoka kwenye maghala ya serikali hapa Marsabit ni jambo ambalo limekuwa likiripotiwa kwa muda mrefu huku baadhi ya maafisa wa serikali wakihusishwa na kashfa hiyo.


Serikali ya Kaunti ya Marsabit ilitangaza kusitisha miradi yote ya maendeleo jimboni hapa ili kuangazia makali ya ukame na kuwasaidia wananchi japo malalamiko yamekuwa yakiibuka kila mara kuhusu usambazaji wa chakula cha msaada.

Post a Comment

0 Comments