TARURA Nachingwea kutumia shilingi 2.94 kwa matengenezo ya barabara.


Na Ahmad Mmow, Lindi. 

Wakala wa barabara za vijijini na mijini(TARURA) wilayani Nachingwea mkoani Lindi inatarajia kutumia jumla ya shilingi bilioni 2.94  kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika mwaka wa fedha wa 2023\2024.  


Hayo yalielezwa jana mjini Nachingwea, na meneja wa TARURA wa wilaya ya Nachingwea, mhandisi Enock Mshiha kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea. 


 Mhandisi Mshiha alisema kwa mwaka wa fedha wa 2023\ 2024  TARURA wilaya ya Nachingwea imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 2.9426 zikiwemo fedha za matengenezo na maendeleo kutoka mfuko wa barabara, fedha za jimbo na tozo ya mafuta kulingana na ukomo wa bajeti uliotolewa kwa ajili ya matengenezo ya barabara mbalimbali zilizopo katika wilaya hiyo. 


 Mshiha alivitaja vyanzo hivyo na kiasi  kinachotarajiwa kupatikana kutokana na vyanzo hivyo kuwa ni  mfuko wa barabara shilingi milioni 942.573, mfuko wa jimbo shilingi milioni 500.00, mfuko wa maendeleo shilingi milioni 500.00 na  tozo ya mafuta shilingi bilioni 1.00. 


Meneja huyo wa TARURA wa wilaya ya Nachingwea alisema  kwa mwaka wa fedha wa 2022\2023 kupitia fedha za matengenezo kutoka mfuko wa barabara, wakala huo umepanga  kufanya matengenezo ya kawaida, sehemu korofi, muda maalumu na ujenzi wa makalavati katika barabara mbalimbali. 


" Kutoka mfuko wa maendeleo wa jimbo, imepanga kufanya matengenezo kwa kiwango cha changarawe, ufungaji wa taa za barabarani na usanifu wa  daraja katika barabara," alisema Mshiha. 

Alizitaja barabara  zitakazofanyiwa matengenezo hayo ya kiwango cha changarawe, kufungwa taa na kufanyiwa usanifu kwa ajili ya ujenzi wa daraja kuwa ni  Lionja-Nditi-Namapwia, Bomani-Matangini-Mpiruka na Posta-Naipingo-Nang'ondo. 

Aidha mhandisi huyo alibainisha kwamba fedha zitakazo tokanana tozo ya mafuta zitatumika kufanya matengenezo ya barabara kwa kiwango cha changarawe na lami. Huku akizitaja barabara hizo kuwa ni SMART LODGE(kiwango cha lami kilometa 0.51), ANGAZA(kiwango cha lami kilometa 0.19) na NAMBAMBO (kiwango cha changarawe kilometa 1.35). 


" Kwa fedha za maendeleo kutoka mfuko wa barabara, TARURA imepanga kufanya matengenezo ya barabara  kwa kiwango cha lami na ujenzi wa boksi kalavati katika barabara za KKT-HOSPITALI kilometa 0.43, VODA kilometa 0.10 na daraja katika barabara ya Mkotokuyana-Chinongwe," alisema mhandisi Mshiha. 


Mtaalamu kiongozi huyo wa ujenzi na matengenezo na ujenzi wa barabara katika wilaya ya Nachingwea alihitimisha kusoma bajeti yake kwakusema hadi Desemba, mwaka 2022  TARURA katika wilaya hiyo ilishapokea jumla ya shilingi 850,363,213.39 kwa ajili ya utekelezaji  wa kazi za matengenezo ya barabara mbalimbali. 

Post a Comment

0 Comments