Viongozi wa dini Kenya wapewa kibarua cha kurejesha umoja

 


Wakati viongozi wanaotawala Kenya wakipishana kwenye nyumba za ibada kushukuru kwa kuchaguliwa na wa upinzani wakiendelea kuhoji kuwa waliibiwa kura, viongozi wa dini wametakiwa kusimama imara kurejesha umoja wa kitaifa.


Akiongoza mkutano wa maombi ya shukrani uliowaleta pamoja viongozi wa kisiasa, mawaziri, viongozi wa kidini na maafisa wakuu wanaohudumu katika kaunti ya Nakuru, Gavana Susan Kihika aliwahimiza viongozi wa kidini kudhihirisha mchango wao kwa umma na kutoa mwongozo unaofaa.


Mchango wa kanisa kwenye siasa umesababisha mdahalo mkubwa nchini Kenya hasa baada ya kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja one Kenya, Raila Odinga, kumkosoa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana, Jackson Ole Sapit, kwa kuhusika kwenye siasa na kuegemea upande wa mpinzani wake, Rais William Ruto, wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.


Kwa upande wake, Askofu Sapit ametoa wito kwa wanasiasa kupunguza cheche zao na badala yake kuzingatia utangamano wa Wakenya na namna ya kuboresha hali ya uchumi wa Wakenya.


Mkuu huyo wa Kanisa la Anglikana nchini Kenya amekuwa akihimiza usawa baina ya viongozi walioko serikalini na wale walio kwenye upinzani.


"Ustawi wa taifa hili ni muhimu kwetu sote. Kenya inahitaji kuimarika kwa kuboresha mahusiano kati yetu, tuvunje misingi ya kikabila na kusonga mbele pamoja. Tunahitaji pia kuimarika kiuchumi, kwa kuangazia mambo yanayowaathiri wakenya kama vile gharama ya juu ya maisha. Lakini tutaweza kufikia haya iwapo kutakuwa na mazingira mazuri ya kisiasa." Alisema Askofu Sapit.


'Kesi mahakamani zakwamisha maendeleo'


Gavana Kihika, ambaye alifunguliwa kesi mahakamani alipoanza tu mchakato wa kuunda serikali yake baada ya kutwaa ushindi kwenye uchaguzi wa Agosti, alisema kesi za mara kwa mara mahakamani zinakwamisha utoaji wa huduma kwa umma.

Post a Comment

0 Comments