Abiria afungiwa kwenye kiti baada ya kumtemea mate mfanyakazi wa ndege

 Wafanyakazi wa shirika la ndege la India walimfunga mwanamke wa Kiitaliano kwenye kiti chake wakati wa safari ya ndege baada ya kudaiwa kumpiga mfanyakazi mmoja na kumtemea mate mwingine.


Mwanamke huyo ambaye alikuwa akisafiri kwa ndege ya Vistara kutoka Abu Dhabi, alikamatwa mjini Mumbai siku ya Jumatatu na baadaye kuachiliwa kwa dhamana ya polisi.


Wakili wake amekanusha madai hayo akisema ni "hadithi ya uwongo". Lakini Vistara alisema wafanyakazi wake walilazimika kumzuia mwanamke huyo kwa "kuendelea tabia chafu na tabia ya ukatili".



Gazeti la The Times of India liliripoti kwamba mfanyakazi wa Vistara alidai katika malalamiko ya polisi kwamba abiria huyo aliwapiga ngumi na kumtemea mate mwenzao.


Kulingana na malalamiko hayo, mfanyakazi huyo alipinga baada ya mwanamke huyo kuacha kiti chake cha daraja la uchumi na kukaa katika daraja la biashara.


Malalamiko hayo pia yanamtuhumu mwanamke huyo kwa "kuvua nguo na kutupa takataka kwenye ndege". Vistara alisema katika taarifa kwamba nahodha wa ndege hiyo "alitoa kadi ya onyo na akafanya uamuzi wa kumzuia mteja" kwa sababu ya tabia yake. Wakili wa mwanamke huyo, Prabhakar Tripathi, aliiambia BBC kwamba "hakuwa na raha" katika kiti chake alichopewa na "aliomba kuhamishwa hadi kwenye kiti kilichokuwa wazi" na hiyo ilisababisha "kutoelewana" na wafanyakazi.


Alisema pia inadaiwa hakuruhusiwa kutumia bafu kutokana na misukosuko. "Baadaye aliruhusiwa kwenda kwenye maliwato lakini alifungwa wakati wa kurudi," Bw Tripathi alisema.


Pia alikanusha ripoti za vyombo vya habari vilivyowanukuu maafisa wa polisi wakisema kuwa mwanamke huyo alikuwa amelewa.


Afisa mkuu wa polisi wa Mumbai aliwaambia waandishi wa habari kwamba mwanamke huyo "amefungiwa kwa utovu wa nidhamu".


"Tulimpa notisi na kumpeleka mbele ya mahakama, na baada ya hapo akaruhusiwa kwenda," alisema Dikshit Gedam, naibu kamishna wa polisi.


Uchunguzi wa utovu wa nidhamu wa abiria wa ndege umeongezeka nchini India baada ya mwanamume mmoja kukamatwa mwezi Januari kwa madai ya kumkojolea abiria wa kike tukio hilo lilizua ukosoaji wa jinsi shirika la ndege la Air India lilivyoshughulikia tukio hilo.

Post a Comment

0 Comments