EWURA, PAU waridhishwa na maendeleo ujenzi wa miundombinu mradi wa EACOP, Tanga



Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Mamlaka ya Petroli Uganda (PAU), imeridhishwa na maendeleo ya awali ya maandalizi ya ujenzi wa miundombinu katika mradi bomba la mafuta EACOP, katika eneo la Chongoleani Tanga. 

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi wa Petroli EWURA, Bw. Gerald Maganga alisema: “Tumeridhishwa na hatua za awali katika uandaaji wa ujenzi wa mradi huu, tumeona maeneo mbalimbali yakiandaliwa kwaajili ya kujenga matanki na miundombinu mingine kwa kuzingatia ushirikishwaji wa wazawa katika kufanya kazi mbalimbali”

Aidha kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Petroli Uganda (PAU), Bw. Ernest Rubondo, amepongeza hatua iliyofikiwa, kwani inaonesha matumaini makubwa katika maendeleo ya ujenzi  wa bomba hilo la mafuta ghafi la Afrika Mashariki.

Inakadiriwa kuwa takribani mapipa 216,000 ya mafuta ghafi yatasafirishwa kwenye bomba hilo kwa siku, kutoka Uganda kwenda kwenye peninsula ya Chongoleani mkoani Tanga, nchini Tanzania ambapo yatajengwa Matanki ya kuhifadhia mafuta, kabla ya kupakiwa kwenye meli kuuzwa katika masoko ya nje.

Bw. Maganga alimalizia kwa kutoa mwito kwa watanzania, kuendelea kujiandikisha katika kanzi data ya EWURA, ili waweze kutoa huduma katika miradi ya gesi na mafuta nchini ikiwemo mradi wa bomba la mafuta la EACOP.

Post a Comment

0 Comments