Facebook: Robo ya watu duniani walitumia mtandao kila siku mwezi Disemba

 


Idadi ya watu wanaotumia Facebook kila siku iliongezeka hadi kufikia wastani wa bilioni mbili mwezi Disemba - karibu robo ya idadi ya watu duniani.


Ukuaji huo mkubwa kuliko ilivyotarajiwa ulisaidia kuleta matumaini mapya kuhusu kampuni, ambayo imekuwa chini ya shinikizo huku gharama zake zikipanda kufuatia kushuka kwa mauzo ya biashara.


Hisa katika kampuni mama ya Meta zilipanda zaidi ya 15% katika biashara ya baada ya saa za kazi huku bosi Mark Zuckerberg alipotangaza 2023 kuwa "mwaka wa ufanisi".


Alisema alijikita katika kupunguza gharama.


"Tuko katika mazingira tofauti sasa," alisema, akiashiria mapato ya kampuni, ambayo yalipungua mnamo 2022 kwa mara ya kwanza katika historia yake baada ya miaka ya ukuaji wa nambari mbili.


"Hatutarajii kwamba hiyo itaendelea, lakini pia sidhani kama itarudi kama ilivyokuwa hapo awali."


Meta, ambayo pia inamiliki Instagram na WhatsApp, ilitangaza marekebisho makubwa mwaka jana, ikiwa ni pamoja na kupunguza nafasi za ofisi na kupunguza ajira 11,000 au karibu 13% ya wafanyakazi.


Kampuni hiyo ilisema hatua hizo ziligharimu dola bilioni 4.6 mwaka jana. Mwaka 2022 ilipata faida ya $23.2bn kwa mwaka.


"2022 ulikuwa mwaka wa changamoto lakini nadhani tulimaliza tukiwa tumepiga hatua nzuri," Bw Zuckerberg alisema.


Meta iliwatia wasiwasi wawekezaji mwaka jana ilipochapisha kupungua kwa mara ya kwanza kwa watumiaji wa Facebook kila siku katika historia yake na kuashiria kuwa ilikuwa inalenga uwekezaji kwenye uhalisia pepe, unaojulikana kama metaverse.


Lakini mnamo Desemba, idadi ya watumiaji kwenye mtandao huo kila siku iliongezeka kwa 4% kutoka mwaka uliopita, na kuongeza watumiaji hata Ulaya na Marekani na Canada.

Post a Comment

0 Comments