Marekani inafuatilia puto inayoshukiwa kuwa ya ujasusi kutoka China

 


Marekani inafuatilia puto inayoshukiwa kuwa ya Uchina ambayo imeonekana ikiruka kwenye maeneo nyeti katika siku za hivi karibuni.


Maafisa wa ulinzi walisema wana uhakika "puto ya uchunguzi wa juu" ni ya China. Ilionekana hivi karibuni juu ya jimbo la magharibi la Montana.


Lakini viongozi wa kijeshi waliamua kutoiangusha kwani kulikuwa na wasiwasi juu ya hatari ya kuanguka kwa vifusi.


China bado haijatoa maoni.


Rais wa Marekani Joe Biden amefahamishwa kuhusu kifaa hicho.


Kitu hicho kiliruka juu ya Visiwa vya Aleutian vya Alaska na kupitia Canada kabla ya kuonekana juu ya jiji la Billings huko Montana siku ya Jumatano, maafisa walisema.


Afisa mkuu wa ulinzi akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina alisema serikali ilitayarisha ndege za kivita, zikiwemo F-22, endapo Ikulu ya White House itaamuru kitu hicho kiangushwe.


Viongozi wakuu wa kijeshi, akiwemo Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin na Jenerali Mark Milley, mwenyekiti wa Wakuu wa Pamoja wa jeshi la Marekani, walikutana Jumatano kutathmini tishio hilo. Bw Austin alikuwa akisafiri Ufilipino wakati huo.


Montana, jimbo la magharibi lenye wakazi wachache, ni nyumbani kwa mojawapo ya maeneo matatu pekee ya kuhifadhi makombora ya nyuklia nchini humo, katika Kambi ya Jeshi la Wanahewa ya Malmstrom, na maafisa walisema chombo hicho cha kijasusi kilikuwa kikiruka juu ya maeneo nyeti kukusanya taarifa.


Afisa wa ulinzi, hata hivyo, alisema hakuna "tishio lililoimarishwa kwa kiasi kikubwa" la ujasusi wa Marekani kuathiriwa kwa sababu maafisa wa nchi hiyo "wanajua puto hii iko wapi na inapita wapi".


Aliongeza kuwa pia hakuna tishio kwa usafiri wa anga wa kiraia kwani kifaa hicho kilikuwa "kwa kiasi kikubwa" juu ya urefu unaotumiwa na mashirika ya ndege ya kibiashara.

Post a Comment

0 Comments