Puto la China: Ndege ya Marekani yalidungua juu ya bahari ya Atlantic

 


Marekani imelidungua puto kubwa la China ambalo inasema limekuwa likifanya ujasusi katika maeneo muhimu ya kijeshi kote Marekani.


Wizara ya Ulinzi imethibitisha kuwa ndege zake za kivita ziliidondosha puto hiyo kwenye eneo la maji ya Marekani.


Wizara ya mambo ya nje ya China baadaye ilieleza "kutoridhishwa na kupinga hatua hiyo dhidi ya utumizi wa nguvu wa Marekani kushambulia ndege za kiraia zisizo na rubani".


Picha kwenye mitandao ya TV ya Marekani zilionyesha puto likianguka baharini baada ya mlipuko mdogo.


Ndege ya kivita aina ya F-22 ililishambulio puto hilo kwa kutumia kombora moja - AIM-9X Sidewinder - na ikaanguka takriban maili sita kutoka pwani ya Marekani saa 14:39 EST (19:39 GMT), afisa wa ulinzi aliiambia. waandishi wa habari.


Maafisa wa ulinzi waliviambia vyombo vya habari vya Marekani kwamba vifusi vya puto hilo vilianguka katika futi 47 (14m) za maji - chini ya walivyotarajia - karibu na Myrtle Beach, South Carolina.


Wanajeshi sasa wanajaribu kurejesha vifusi ambavyo vimetapakaa zaidi ya maili saba (11km). Meli mbili za wanamaji, ikiwa ni pamoja na moja yenye korongo nzito kwa ajili ya uokoaji, ziko katika eneo hilo.


Katika taarifa ya Pentagon afisa mkuu wa ulinzi wa Marekani alisema kuwa "wakati tulichukua hatua zote muhimu ili kulinda dhidi ya ukusanyaji wa taarifa nyeti wa PRC [China], puto ya uchunguzi ya juu ya ardhi ya Marekani ilikuwa ya muhimu sana .


"Tuliweza kusoma na kuchunguza puto na vifaa vyake, ambavyo vimekuwa vya thamani," afisa huyo aliongeza.


Rais wa Marekani Joe Biden alikuwa chini ya shinikizo la kuangusha puto hiyo tangu maafisa wa ulinzi walipotangaza kwa mara ya kwanza kuwa wanaifuatilia siku ya Alhamisi.


Baada ya puto kudunguliwa, Bw Biden alisema: "Walifanikiwa kuliangusha, na ninataka kuwapongeza waendeshaji wa ndege wetu waliofanya hivyo."


Katika taarifa yake saa chache baadaye, wizara ya mambo ya nje ya China ilisema: "Upande wa China mara kwa mara umefahamisha upande wa Marekani baada ya kuthibitisha kwamba ndege hiyo isio na rubani ilikuwa ni ya matumizi ya kiraia na iliingia Marekani kutokana na kulazimishwa kwa nguvu - ilikuwa ajali kabisa."


Kugunduliwa kwa puto hilo kulizua mzozo wa kidiplomasia, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisitisha mara moja safari ya mwishoni mwa wiki hii nchini China kutokana na "kitendo cha kutowajibika".


Mamlaka ya Uchina imekanusha kuwa ni ndege ya kijasusi, na badala yake ilisema ilikuwa meli ya hali ya hewa iliyopulizwa.


Ikijibu tukio hilo, wizara ya mambo ya nje ya Taiwan ilisema katika taarifa yake: "Hatua za serikali ya Chama cha Kikomunisti cha China zinazokiuka sheria za kimataifa na kukiuka anga na mamlaka ya nchi nyingine hazipaswi kuvumiliwa katika jumuiya ya kimataifa iliyostaarabika."


China inaichukulia Taiwan inayojitawala yenyewe kuwa jimbo lililojitenga ambalo hatimaye litakuwa chini ya udhibiti wa Beijing. Rais Xi Jinping hajakataza uwezekano wa matumizi ya nguvu kufanikisha hili.


Lakini Taiwan inajiona kuwa huru, ikiwa na katiba yake na viongozi waliochaguliwa kidemokrasia.


Rais Biden aliidhinisha kwanza mpango wa kuangusha puto siku ya Jumatano, lakini Pentagon ilisema imeamua kusubiri hadi kitu hicho kiwe juu ya maji ili kutoweka watu chini katika hatari isiyofaa.


Msingi wa operesheni hiyo uliwekwa wakati Utawala wa Shirikisho la Usafiri wa Anga wa Marekani (FAA) ulipositisha kwa muda safari zote za ndege za raia katika viwanja vitatu vya ndege karibu na pwani ya Carolina Kusini Jumamosi alasiri kwa sababu ya "juhudi za usalama wa taifa".


Mlinzi wa pwani pia aliwashauri mabaharia kuondoka eneo hilo kutokana na operesheni za kijeshi "ambazo ni hatari kubwa".


Shahidi aliyeshuhudia ufuo huo, Hayley Walsh, aliambia BBC kwamba aliona ndege tatu za kivita zikizunguka kabla ya kombora kurushwa, kisha "tulisikia sauti kubwa, nyumba ikatikisika".




Afisa mmoja mkuu wa jeshi aliiambia CNN uokoaji wa vifusi unapaswa kuwa "rahisi sana" na unaweza kuchukua "muda mfupi". Afisa huyo aliongeza kuwa "wapiga mbizi wenye uwezo wa Navy" wanaweza kutumwa kusaidia katika operesheni hiyo.


Maafisa wa ulinzi pia walifichua Jumamosi kwamba puto hilo liliingia kwenye anga ya Marekani tarehe 28 Januari karibu na Visiwa vya Aleutian, kabla ya kuhamia anga ya Canada siku tatu baadaye, na kuingia tena Marekani tarehe 31 Januari. Kitu hicho kilionekana katika jimbo la Montana nchini Marekani, ambalo ni nyumbani kwa maeneo kadhaa nyeti ya makombora ya nyuklia.


Uhusiano kati ya China na Marekani umeathiriwa na tukio hilo, huku Pentagon ikilitaja kuwa "ukiukaji usiokubalika" wa uhuru wa Marekani.


Bw Blinken - mwanadiplomasia mkuu wa Marekani - aliiambia Beijing "kitendo cha kutowajibika" kabla ya safari yake ambayo sasa imeahirishwa hadi tarehe 5-6 Februari - ingekuwa mkutano wa kwanza wa ngazi ya juu kama huo wa Marekani na China kwa miaka mingi.


Lakini China ulitaka kuahirisha ziara yake, ikisema katika taarifa yake Jumamosi kwamba hakuna upande uliotangaza rasmi mpango wa safari.


Wizara ya mambo ya nje ya China ilisema Beijing "haitakubali dhana yoyote isiyo na msingi au porojo" na ikashutumu "baadhi ya wanasiasa na vyombo vya habari nchini Marekani" kwa kutumia tukio hilo "kama kisingizio cha kushambulia na kuipaka matope China."


Siku ya Ijumaa, Pentagon ilisema puto ya pili ya kijasusi ya Uchina imeonekana - wakati huu katika eneo la Amerika ya Kusini na kuripotiwa kuonekana juu ya Costa Rica na Venezuela.


Jeshi la Wanahewa la Colombia linasema kitu kilichotambuliwa - kinachoaminika kuwa puto - kiligunduliwa mnamo 3 Februari katika anga ya nchi hiyo kwa zaidi ya futi 55,000.


Inasema ilifuata kitu hicho hadi ilipoondoka kwenye anga, na kuongeza kuwa haikuwakilisha tishio kwa usalama wa taifa.


China bado haijatoa maoni hadharani kuhusu puto ya pili iliyoripotiwa.



Post a Comment

0 Comments