https://monetag.com/?ref_id=TTIb NEMC yang’ara kimataifa maonesho ya kilimo na mazingira Qatar | Muungwana BLOG
https://monetag.com/?ref_id=TTIb

NEMC yang’ara kimataifa maonesho ya kilimo na mazingira Qatar

 


Tanzania ni miongoni mwa nchi 130 zinazoshiriki Maonesho  ya Kimataifa ya Kilimo na Mazingira(Agriteq Expro 2023) ambayo  hufanyika kila mwaka na  kwa mwaka huu  yanafanyika kuanzia tarehe 15 hadi 19 Machi, 2023  katika jiji la Doha nchini Qatar huku Baraza la Taifa la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) likionesha uzoefu wake kwenye masuala mbalimbali ikiwamo utokomezaji wa mifuko ya plastiki.


 
Katika maonesho hayo yaliyofunguliwa na Waziri wa Manispaa, Dk.  Abdullah bin  Abdulaziz bin Turki Al Subaie na yamejumuisha kampuni za kimataifa  zaidi ya 300, wakulima  zaidi ya 100 pamoja na wadau wa mazingira huku NEMC ikiwa miongoni mwa taasisi 16 zilizoshiriki kutoka Tanzania.

 
Akizungumza katika maonesho hayo,  Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa NEMC, Irene John alisema maonesho hayo yatafungua fursa nyingi za uwekezaji  katika bidhaa na huduma kupitia mawasilisho  yaliyofanywa na NEMC imeonesha jinsi gani mazingira ya uwekezaji yameboreshwa kupitia mifumo mbalimbali ya kielektroniki kama vile mchakato wa  utoaji vibali  vya Tathimini ya Athari kwa Mazingira (TAM)  na pia mfumo wa upatikanaji wa vibali vya taka hatarishi  ili kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji.

“Miongoni mwa wageni waliotembelea banda la NEMC ni pamoja na  watumishi kutoka Ubalozi wa  Tanzania nchini  Qatar, Wizara na kampuni mbalimbali kutoka nchi washiriki, mwananchi mmoja mmoja kutoka Qatar na nchi mbalimbali walitembelea banda la NEMC ikiwa ni pamoja na wawekezaji wa aina mbalimbali  ili kupata elimu  pamoja na kuelezwa fursa za uwekezaji kwenye mazingira, utalii na kilimo,”alisema.


Kadhalika, Ofisa Mazingira kutoka  NEMC  Kanda ya Kusini, Obasanjo Nniwako  alieleza  kuwa moja ya faida kubwa kwa  NEMC kushiriki katika maonesho  ya kimataifa ya  mazingira na kilimo ni pamoja na kuitangaza  NEMC na pia kutoa elimu juu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa uwekezaji endelevu.


“Lakini pia tumeeleza jinsi Tanzania ilivyotokomeza matumizi ya mifuko ya Plastiki na kuonesha kwa vitendo baadhi ya mifuko mbadala  inayotumika ambayo ni rafiki kwa Mazingira  kwa ajili ya maendeleo endelevu  kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,”alisema.

Naye, Tilisa Mwambungo Afisa Mazingira toka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, aliongeza kuwa kwenye maonesho wanatangaza  fursa  zilizopo  za uwekezaji  hasa katika kilimo  endelevu  kinachozingatia  uhifadhi  wa mazingira  pamoja na utalii kwa ajili ya  kukuza uchumi wa nchi  na kuongeza ajira.

“Kwa ujumla wake, maonesho yametoa fursa kwa washiriki kutoka  Tanzania    kueleza Mataifa  juu ya  maeneo  mbalimbali ya uwekezaji nchini Tanzania, hususani katika sekta ya kilimo,  ufugaji, utalii na madini  ambazo zinapatikana  nchini Tanzania na NEMC imeweza  kutoa elimu kwa washiriki  waliotembelea banda letu kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa  wakati wa kufanya tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya kuwekeza nchini Tanzania,”alisema.

 Maonesho hayo yanalenga kutoa  fursa kwa washiriki  kuonesha bidhaa na huduma zinazohusiana na kilimo na mazingira, kubadilishana uzoefu,  teknolojia  pamoja  kutafuta masoko na fursa na uwekezaji katika kilimo  kinachozingatia  uhifadhi wa mazingira.

Mbali na NEMC, washiriki wengine kutoka nchini Tanzania  ni pamoja na Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania -Qatar,  Wizara ya Kilimo, Bodi ya Mkonge, Mama  Afrika, SL. Afrika, Dumas Afrikan Market, Msai Sandals, Habimaya Solutions, Natural Shine Trader, Nkona Limited, Linga Enterprises, MamboJambo Design,  Kolumba Art Studio, Afnaan Limted  pamoja na  Amahoro  Afrika Limited.

 

Post a Comment

0 Comments