Rwanda: Jinsi mtoro mmoja kati ya wanaosakwa kwa mauaji ya halaiki alivyopatikana amejificha Cape Town


"Ilikuwa operesheni kubwa na ya muda mrefu" msemaji wa polisi Brigedia Thandi Mbambo anaiambia BBC, kuhusu kukamatwa kwa mtoro wa kwanza kati ya wanne waliokuwa wakisakwa zaidi nchini Rwanda kwa mauaji ya halaiki mwaka 1994 siku ya Jumatano.


Fulgence Kayishema, 61, "ametumia vitambulisho vingi vya uongo, na wakati wa kukamatwa kwake alipatikana akijiita Donatien Nibashumba", Brig Mbambo anasema.


Alikuwa akitafutwa kwa madai ya kuhusika moja kwa moja na mauaji ya Watutsi zaidi ya 2,000 katika kanisa katoliki na kutumia tingatinga kuangusha kanisa hilo na kuwazika ndani baadhi ya watu baada ya juhudi za kuliteketeza kanisa hilo huku watu wakiwa ndani kushindikana.


Kasisi wa kanisa hilo likiwa na watu, Athanase Seromba, alihukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka wa 2008.


Kayishema mwendesha mashtaka wa zamani wa eneo hilo magharibi mwa Rwanda, "alikuwa akifanya kazi kama kibarua katika shamba kubwa" huko Paarl karibu kilomita 60 magharibi mwa Cape Town.


"Wakati anakamatwa, alikuwa anakaa peke yake, familia yake iko Cape Town, kuna mambo fulani ambayo yatachunguzwa, lakini alikuwa anakaa peke yake shambani." Brig Mbambo alisema.


Vyama vya manusura wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda vimeelezea kuridhishwa na kukamatwa kwa Kayishema na kutaka haki ichukue mkondo wake.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kukamatwa kwa Kayishema "kunatuma ujumbe mzito kwamba wale wanaodaiwa kufanya uhalifu huo hawawezi kukwepa haki".


Polisi wa Afrika Kusini waliongoza uchunguzi na operesheni iliyoanza mwaka 2022 iliyohusisha polisi na mamlaka kutoka Canada, Eswatini, Msumbiji, Rwanda, Marekani na Uingereza ili kumpata mshukiwa.


"Vyombo vyote hivyo vililazimika kuchukua jukumu la kujumuisha taarifa zote pamoja hadi hatimaye wakawa na uhakika wa 100% kuwa huyu ndiye mtu wanayemtafuta" Brig Mbambo anasema.


Anaongeza kuwa mshukiwa alifanikiwa kuja na kukaa Afrika Kusini kwa kutumia vitambulisho bandia na "kuishi maisha ya utulivu sana shambani, akijaribu kuhakikisha kuwa hakuna anayemjua yeye ni nani."


Siku ya Ijumaa, Bw Kayishema anatarajiwa kufikishwa mahakamani mjini Cape Town kuhusu sheria za uhamiaji na ilani ya Interpol akisubiri kupelekwa Rwanda, polisi walisema kwenye tovuti yake.

Post a Comment

0 Comments