Serikali yazindua miongozo na nyaraka za Elimu ya Awali


SERIKALI imezindua miongozo na nyaraka za Elimu ya Awali zitakazorahisisha utoaji wa huduma stahiki kwa watoto kwenye malezi na ujifunzaji ili kujenga makuzi timilifu.

Uzinduzi huo umefanyika Mei 26, 2023 na Mkurugenzi Msaidizi Ithibati Shule, Patrick Leyana kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda katika Shule ya Msingi Mtemi Mazengo jijini Dodoma.

Amesema miongozo na nyaraka hizo zimeandaliwa ili kuwawezesha wadau wa elimu ya awali kutoa huduma kwa watoto wote kwa usawa na kwa kuzingatia mahitaji yao.

Ametaja miongozo hiyo kuwa ni pamoja na Mwongozo wa Kitaifa wa Uendeshaji na Viwango katika Elimu ya Awali (MUVEA), Kiongozi cha Utekelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Uendeshaji na Viwango katika Elimu ya Awali (KUMUVEA), Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji na Utekelezaji wa Shughuli za Ushirikiano wa Wazazi na Walimu katika Elimu ya Awali na Msingi.

Mingine ni Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji, Usimamizi na Uendeshaji wa Vituo Shikizi vya Shule pamoja na Mwongozo wa Upimaji Shirikishi wa Matokeo ya Ujifunzaji kwa Wathibiti Ubora wa Shule.

“Shukrani za pekee kwa Shirika la Kimataifa la Watoto Duniani UNICEF na GPE LANES II pamoja na mashirika mengine likiwemo shikrika la Children in Crossfire Watoto wetu Tunu Yetu, USAID- Jifunze Uelewe na UKaid-Shule Bora mliochangia kwa moyo wa dhati kufanikisha uandaaji, uchapaji na uzinduzi wa miongozo hii,”amesema.

Amewaomba viongozi wengine kutoka katika wizara zinazohusika na masuala ya watoto kutumia miongozo hiyo ili kuwezesha upatikanaji wa huduma jumuishi kwa watoto wote wakiwemo wenye mahitaji maalumu kufikia viwango vya ubora wa kitaifa, kikanda na kimataifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu ya Awali na Msingi kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Bi.Susan Nussu, amesema miongozo hiyo itasaidia kujenga elimu bora kwa watoto wa kitanzania wakiwa na umri mdogo na kupitia mradi wa BOOST walimu 3,000 watafikiwa kujengewa uwezo wa kufundisha madarasa ya awali.

Awali Mratibu wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Hawa Selemani, amesema miongozo hiyo itaweka viwango vya ubora katika utekelezaji wa elimu ya awali.

Naye Mtaalamu wa masuala ya Elimu kutoka Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Audax Tibubinda, amesema hatua hiyo inaonesha hatua kubwa katika maendeleo ya elimu na kuhimiza wataalamu wa ndani waendelee kutumika zaidi ili kuleta mafanikio ya aina hiyo.

 


Post a Comment

0 Comments