Wanawake zaidi ya 200 washiriki mbio za Mamathon Korogwe


 Na Mwandishi Wetu Tanga

WANAWAKE wajawazito zaidi ya 2000 wilayani Korogwe mkoani Tanga  wameshiriki katika mbio za Mamathon ambazo zimefanyika kwa mara ya kwanza wilayani humo zilizoandaliwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo.

Lengo la kufanyika kwa Mamathon ni kutoa hamasa kwa wanawake wajawazito kujifungua salama na hatimaye kupunguza vifo vya mama na mtoto kama ambavyo Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

Akizungumza leo Mei 28, 2023 mbele ya wanawake hao,  wananchi pamoja na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Wilaya ya Korogwe , Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Mary Chatanda aliyekuwa mgeni rasmi amempongeza Jokate kwa ubunifu huo.

"Tunakupongeza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na kote alikopita amekuwa akifanya kazi nzuri hivyo wananchi wa Wilaya ya Korogwe wajue wamepata jembe na ndio maana Rais Dkt Samia Hassan Suluhu ameendeea kumteua katika nafasi hiyo ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe .

"Wananchi wa Korogwe mmepata jembe na muendelee kumpa ushirikiano na sisi viongozi tutaendelea kumuunga mkono na katika hili la ambalo ameliazisha aendelee nalo kwani linagusa maisha ya wamama wajawazito na watoto moja kwa moja kulinda afya zao, " amesema Chatanda.

Pia amewataka wananchi wa Korogwe kumtumia Mkuu wa Wilaya hiyo kwani ana mambo mazuri yatakayowezesha kuwaletea maendeleo na wao kama viongozi wa Chama na Serikali watatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha anatekeleza majukumu yake vizuri.

Akifafanua kuhusu mbio za Mamathon amesema ni jambo jipya katika Wilaya ya Korogwe na Jokate ameonesha  ubunifu mkubwa,  hivyo anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mkuu huyo wa Wilaya kwani mambo yamekuwa moto.

 Aidha amewapongeza wanawake wajawazito pamoja na wote walioshiriki na kumaliza mbio hizo kwani kufanya mazoezi kwa mjazito kuna faida nyingi."Kupitia mbio hizi kuna mama mjamzito mmoja amepelekwa hospitali na tunamuombea ajifungue salama."

Amewataka kuhakikisha baada ya mbio hizo wanaendelea kushiriki mazoezi ,kuzingatia lishe Bora kipindi chote cha ujauzito wao jambo litakalosaidia  kujifungua salama na kuwezesha mpango wa Serikali wa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga.

Pamoja na mambo mengine Chatanda amesema mbali ya mbio hizo,  amepokea vifaa tiba kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Korogwe na hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kuboresha huduma za afya ikiwemo ununuzi wa dawa na vifaa tiba.

"Kuna kila sababu ya kumpongeza Rais Dkt Samia Kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta ya afya na kwa kipindi cha miaka miwili kwa nchi nzima ameboresha  miundombinu kwenye sekta ya afya katika ngazi zote za Zahanati ,vituo vya afya ,Hospitali za Wilaya , na kungineko na kupeleka vifaa tiba kwa ajili ya kutolea huduma za afya."

Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wahudumu katika vituo vya afya Zahanati ,na Hospitali zote kuzingatia maadili ya kazi zao na kuepuka na vitendo vinavyokwenda  kinyume na maadili ya kazi wanayoifanya huko akitolea mfano vitendo vilivyojitokeza wilayani Kaliua mkoani Tabora na anashukuru Mkuu wa Mkoa wa Tabora Baltida Burhan kwa kuchukua hatua.

Post a Comment

0 Comments