Israel imetoa onyo jipya kwa raia wa Gaza walioko Khan Younis kusini mwa eneo hilo kuondoka.
Siku tatu baada ya Israel kuangusha vipeperushi vya kuwaonya watu kuondoka Khan Younis, onyo jingine la kuhama mji huo limetolewa.
Khan Younis ndio mji mkubwa zaidi kusini mwa Gaza - ambapo mamia ya maelfu ya watu walikimbilia baada ya kuambiwa wahame kaskazini.
Huku mzozo wa kibinadamu ukizidi kuwa mbaya katika jiji hilo lililojaa watu wengi, onyo la Israel lilidokeza kwamba operesheni za kijeshi ziko karibu.
Mark Regev, mshauri wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, aliviambia vyombo vya habari vya Marekani wakati wanajeshi wa Israel watalazimika kuingia mjini humo kuharibu mahandaki ya Hamas, watu wa Khan Younis wanaweza kuhamia magharibi, "Ambapo kwa matumaini kutakuwa na mahema na uwanja hospitali”.
"Nina hakika kwamba hawatalazimika kuhama tena" ikiwa watahamia magharibi, alisema.
Mamia ya maelfu ya watu wa Gaza walikimbia kaskazini kuelekea maeneo ya kusini ikiwa ni pamoja na Khan Younis baada ya kuamriwa kuondoka na Israel kwa usalama wao. Lakini eneo la kusini limeendelea kuwa chini ya mashambulizi ya Israel pia.
