Malipo kwa maafisa wa polisi na magereza nchini Kenya yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 40 katika kipindi cha miaka mitatu kufuatia mapendekezo ya mapitio ya sekta ya usalama, Rais William Ruto amesema.
Nyongeza ya mishahara inakusudiwa kuongeza ari na kuimarisha usalama.
Ilikuwa ni moja ya mapendekezo yaliyotolewa na jopo kazi linaloangalia jinsi ya kuboresha ulinzi wa polisi nchini.
Polisi wa Kenya wana sifa ya ukatili na hongo, lakini pia kumekuwa na wasiwasi kuhusu ustawi wao.
Wanalipwa pesa kidogo na wengine wameishia kugeukia uhalifu wenyewe. Polisi kadhaa wamejiua katika miaka ya hivi karibuni na ukweli kwamba wengi wanahangaika na afya yao ya akili umetambuliwa.
Hapo awali kumekuwa na hatua za kuongeza malipo yao lakini haijaleta mabadiliko makubwa jinsi Wakenya wanavyowachukulia.
Habari za nyongeza hiyo ya mishahara inajiri huku Kenya ikikabiliana na mzozo wa gharama ya maisha ambao umesababisha serikali kuongeza ushuru na tozo mbalimbali.
