Wizara ya sheria ya Urusi imewasilisha ombi kwa Mahakama ya Juu Zaidi ya nchi hiyo kupiga marufuku shughuli za kile inachokiita "vuguvugu la kimataifa la LGBT" kama lenye itikadi kali.
Haiko wazi kama taarifa ya wizara inarejelea jumuiya ya LGBT kwa ujumla au mashirika maalum.
Ilisema vuguvugu hilo limeonyesha dalili za "shughuli zenye itikadi kali", ikiwa ni pamoja na kuchochea "migogoro ya kijamii na kidini".
Marufuku hiyo inaweza kumwacha mwanaharakati yeyote wa LGBT katika hatari ya kufunguliwa mashitaka ya jinai.
Hatua hiyo yenye msimamo mkali imekuwa ikitumiwa hapo awali na mamlaka ya Urusi dhidi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu na makundi ya upinzani kama vile Wakfu wa Kupambana na Ufisadi wa Alexei Navalny.
Mahakama ya Juu Zaidi itachunguza ombi hilo tarehe 30 Novemba.
Marufuku hiyo ingefanya mashirika ya LGBT kutoweza kufanya kazi na kuwaweka wanaharakati na wafanyikazi katika hatari ya kufunguliwa mashtaka ya jinai, gazeti la Moscow Times lilimnukuu mmoja wa wanaharakati wachache wa LGBT ambaye bado wako ndani ya Urusi akisema.
"Kimsingi, itahusisha mashtaka ya jinai kwa kuzingatia tu mwelekeo au utambulisho wa mtu."
